Watoto 32 waaga dunia katika mkanyagano kwenye tamasha la wanafunzi nchini Nigeria
Kamanda wa Polisi katika jimbo la Oyo nchini Nigeria, Adewale Osifeso, amesema kuwa watoto wasiopungua 32 wamethibitishwa kufariki dunia katika mkanyagano wa jana kwenye tamasha la wanafunzi jimboni humo.
Ajali hiyo ilitokea jana katika shule ya upili ya Kiislamu ya Bashorun katika makao makuu ya jimbo hilo, huko Ibadan.
Polisi katika jimbo la Oyo imeeleza kuwa, uchunguzi unaendelea kubaini idadi kamili ya waliopoteza maisha katika mkanyagano wa jana.
Vyombo vya habari vimeripoti kuwa tamasha hilo la wanafunzi lilikuwa limeandaliwa na taasisi isiyo ya kiserikali inayojishughulisha na ulinzi na kutoa misaada kwa wanawake; mwanzilishi wake akiwa ni Naomi Silekunola. Polisi inaendelea kumhoji mwasisi wa taasisi hiyo.
Mmoja wa mashuhuda aliyefika katika tamasha hilo aliyejitambulisha kwa jina la Omolewa Azeez ambaye alifika tamashani na mwanae wa kiume wa miaka saba, amesema kuwa alikuta umati mkubwa wa watu wakijaribu kuingia sehemu ya tamasha, hata hivyo hakukuwa na askari usalama wa kutosha. "Watu wengi walianguka na kukanyagwa na wengine walizimia kutokana na msongamano mkubwa wa watu", amesema shuhuda huyo.
Kulingana na matangazo ya redio ya hafla hiyo, waandaaji walitangaza kuwa watagawa chakula na zawadi kwa watoto 5,000 lakini karibu watoto 8,000 walijitokeza mapema saa kumi na moja asubuhi, jana Jumatano.