Malawi inadai mabilioni ya dola kutoka kwa kampuni ya madini ya Marekani
Serikali ya Malawi inadai dola bilioni 309 za kodi na mrabaha ambazo hazijalipwa kutoka kwa kampuni ya Marekani ya Columbia Gem House kwa ajili ya mawe ya thamani yaliyouzwa nje katika muongo mmoja uliopita.
Thabo Chakaka Nyirenda mwanasheria mkuu wa Malawi amesema kwamba nchi hiyo pia inatafuta dola bilioni 4 katika mapato ambayo hayajalipwa kutoka kampuni kubwa ya mafuta ya Ufaransa ya TotalEnergies, pamoja na dola milioni 9.5 kutoka kwa kampuni ya tumbaku ya Star Agritech ya Uturuki.
Kiasi kinachotafutwa kutoka kwa mashirika hayo matatu kinaripotiwa kuwa karibu mara 300 ya deni la taifa la Malawi la takriban dola bilioni 1.2. Mwaka jana, nchi hiyo ilipokea mkopo wa takriban dola milioni 178 kutoka kwa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) huku kukiwa na mzozo wa kiuchumi.
Nchi hiyo isiyo na bahari ina madini mengi kama vile fosfati, makaa ya mawe, chokaa, urani, madini ya chuma, na vito vya thamani. Hata hivyo, takwimu rasmi zimefichua kuwa sekta ya madini inachangia 1% tu katika Pato la Taifa la Malawi. Serikali inalenga ongezeko la hadi 10% ifikapo 2063.
Kampuni ya Columbia Gem House yenye makao yake makuu nchini Marekani imepuuzilia mbali madai hayo ikibainisha kuwa takwimu hizo zina dosari.
Ubalozi wa Marekani nchini Malawi umefanya jaribio la kusuluhisha mzozo huo lakini haukufaulu.
TotalEnergies iliripotiwa kukataa kutoa maoni yake kuhusu madai kwamba imeshindwa kuheshimu makubaliano ya 2001 na Malawi ya kusambaza mafuta badala ya motisha ya kodi.
Star Agritech International (SAI), ambayo pia inashutumiwa na mamlaka ya Malawi kwa kukataa kulipia tani milioni tatu za tumbaku yenye thamani ya dola milioni 15 ambazo ilinunua kutoka Malawi kupitia kampuni tanzu tatu zilizosajiliwa Mauritius, Hong Kong, na Afrika Kusini mwaka 2013, nayo pia imekanusha madai hayo..