Ramaphosa: Waafrika Kusini si wachukia wageni
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i138896-ramaphosa_waafrika_kusini_si_wachukia_wageni
Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, amemweleza mwenzake wa Kenya, Rais William Ruto, kwamba maandamano ya hivi karibuni dhidi ya uhamiaji haramu nchini humo hayamaanishi kuwa Waafrika Kusini wana chuki dhidi ya wageni.
(last modified 2026-06-05T03:00:05+00:00 )
Jun 05, 2026 02:57 UTC
  • Rais wa Kenya William Ruto, na Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini
    Rais wa Kenya William Ruto, na Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini

Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, amemweleza mwenzake wa Kenya, Rais William Ruto, kwamba maandamano ya hivi karibuni dhidi ya uhamiaji haramu nchini humo hayamaanishi kuwa Waafrika Kusini wana chuki dhidi ya wageni.

Ruto yuko katika ziara ya kitaifa ya siku tatu, ambapo mikataba minne mikubwa ya ushirikiano kati ya Pretoria na Nairobi inatarajiwa kutiwa saini ili kuimarisha mahusiano na kukuza sekta za utalii za mataifa hayo mawili.

“Waafrika Kusini si wachukia wageni. Waafrika Kusini ni Waafrika,” Ramaphosa alisema kabla ya kuhitimisha hotuba yake ya mapokezi Alhamisi.

Aliongeza kuwa Waafrika Kusini “wanataka kuishi kwa amani na Waafrika wenzao, na wananchi wetu wanatuhimiza sisi viongozi kutafuta suluhisho la changamoto nyingi zinazotokana na suala la uhamiaji.”

Ramaphosa amemfahamisha Rais Ruto kwamba: “Kama Afrika Kusini, tunalishughulikia suala hili, na nimefurahi kuona kwamba nawe una uelewa mzuri kuhusu changamoto hii. Kwa kufanya kazi pamoja, Afrika Kusini na Kenya zinaweza kusaidia kuunda bara la Afrika lenye amani, lililounganishwa na lenye ustawi, ambalo lina uwezo wa kutatua matatizo yake lenyewe."

Akijibu, Rais Ruto amesema kuna haja kwa nchi za Afrika kuhakikisha kuwa fursa zinapatikana ndani ya bara.

“Sehemu ya changamoto ambayo Afrika Kusini inakabiliana nayo ni kwamba ni nchi iliyoendelea zaidi katika Afrika, na hivyo ni rahisi kwa watu kuja hapa kutafuta huduma na fursa. Suluhisho la hilo ni kuhakikisha kuwa huduma na fursa zinapatikana kila mahali katika bara letu.”

Rais huyo wa Kenya aliongeza: “Naelewa kikamilifu hali inayotokea pale watu wanaposhindania rasilimali na fursa. Ni wajibu wetu kuhakikisha tunaunda fursa katika kila pembe ya bara letu.”

Afrika Kusini imekuwa ikishuhudia wimbi la maandamano dhidi ya uhamiaji haramu. Katika siku za hivi karibuni, polisi walisema raia wawili wa Msumbiji waliuawa katika mji wa Mossel Bay mwishoni mwa juma.

Wakati huo huo, mapema wiki hii, Malawi ilitangaza kuwa itaanza mchakato wa kuwarejesha kwa hiari raia wake walioko Afrika Kusini. Mwezi uliopita, raia 300 wa Ghana walirejeshwa kutoka Afrika Kusini.