Rais mpya wa Ghana ateuwa mawaziri wake wa awali
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i121276-rais_mpya_wa_ghana_ateuwa_mawaziri_wake_wa_awali
Rais mpya wa Ghana, John Dramani Mahama, ameweka wazi uteuzi wake muhimu katika baraza la mawaziri la serikali ijayo ya nchi hiyo kwa kuwateuwa Cassiel Ato Forson kuwa Waziri wa Fedha, John Abdulai Jinapor Waziri wa Nishati, na Dominic Akuritinga Ayine kuwa Mwanasheria Mkuu na Waziri wa Sheria.
(last modified 2025-01-11T02:56:25+00:00 )
Jan 11, 2025 02:56 UTC
  • Rais mpya wa Ghana ateuwa mawaziri wake wa awali

Rais mpya wa Ghana, John Dramani Mahama, ameweka wazi uteuzi wake muhimu katika baraza la mawaziri la serikali ijayo ya nchi hiyo kwa kuwateuwa Cassiel Ato Forson kuwa Waziri wa Fedha, John Abdulai Jinapor Waziri wa Nishati, na Dominic Akuritinga Ayine kuwa Mwanasheria Mkuu na Waziri wa Sheria.

Mahama ambaye aliapishwa kuiongoza Ghana Jumanne iliyopita aliahidi wakati wa kampeni za uchaguzi kuwateua mawaziri wote wa baraza la mawaziri katika siku 14 za kwanza baada ya kuingia madarakani ili kukabiliana na ufisadi. 

Mahama ambaye aliwahi kuwa Rais wa Ghana kuanzia mwaka 2012 hadi 2017, ameahidi kutoa kipaumbele kwa suala la kuhuisha uchumi wa nchi, amani na ustawi wa wananchi pamoja na kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji na kupambana na ufisadi.

Chama cha Mahama cha National Democratic Congress (NDC) kinadhibiti thuluthi mbili ya kura za uwakilishi bungeni jambo ambalo litarahisisha kupitishwa kwa mawaziri aliowateuwa.

Cassiel Ato Forson aliye na umri wa miaka 46 ambaye ameteuliwa kuwa Waziri wa Fedha, kitaaluma ni mhasibu na aliwahi kuwa Naibu Waziri wa Fedha katika muhula wa kwanza wa urais wa Mahama.

John Abdulai Jinapor mwanasiasa na waziri wa zamani wa nishati katika kipindi cha kwanza cha Urais wa Mahama, ameteuliwa kuongoza Wizara ya Nishati.