Maveterani 2 Zimbabwe wakamatwa kwa kumkosoa Rais Mugabe
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i12172-maveterani_2_zimbabwe_wakamatwa_kwa_kumkosoa_rais_mugabe
Polisi ya Zimbabwe inawashikilia mashujaa wawili wa vita vya uhuru nchini humo, wiki moja baada ya maveterani hao kusema kuwa Rais Robert Mugabe wa nchi hiyo ni dikteta na kumtaka ajiuzulu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 28, 2016 11:02 UTC
  • Maveterani 2 Zimbabwe wakamatwa kwa kumkosoa Rais Mugabe

Polisi ya Zimbabwe inawashikilia mashujaa wawili wa vita vya uhuru nchini humo, wiki moja baada ya maveterani hao kusema kuwa Rais Robert Mugabe wa nchi hiyo ni dikteta na kumtaka ajiuzulu.

Maveterani hao Victor Matemadanda na Douglas Mahiya wanatuhumiwa kukiuka sehemu ya 22 ya sheria ya nchi inayotaka kuheshimiwa serikali iliyochaguliwa kwa mujibu wa katiba na sehemu ya 33 inayokataza kuvunjiwa heshima ofisi ya rais.

Kwa mujibu wa Jumuiya ya Mawakili wa Haki za Binadamu nchini Zimbabwe, Douglas Mahiya, msemaji wa Chama cha Maveterani alikamatwa na kuzuiliwa baada ya kujisalimisha katika kituo cha polisi alipotakiwa kufanya hivyo na vyombo vya dola. Jumuiya hiyo imeongeza kuwa, Victor Matemadanda, Katibu Mkuu wa Chama cha Maveterani amekamatwa leo na maafisa wa polisi akiwa nyumbani kwake katika mkoa wa Midlands na kupelekwa katika kituo cha polisi mjini Harare.

Maandamano ya kumuunga mkono Rais Robert Mugabe wa Afrika Kusini

Haya yanajiri siku chache baada ya Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe kuwaonya maveterani wa vita wanaomkosoa akieleza kwamba, watakabiliwa na adhabu kali endapo hawataachana na msimamo wao wa kukataa kuunga mkono serikali yake kufuatia mporomoko mkubwa wa uchumi wa hivi sasa ambao haujawahi kushuhudiwa nchini humo.

Aidha Mugabe ameonya kuwa wale ambao wanaendeleza maandamano dhidi ya serikali huenda wakafungwa jela kwani taifa hilo halina haja ya mapigano ya wenyewe kwa wenyewe.

Maandamano dhidi ya Rais Mugabe

Hivi karibuni maveterani wenza wa Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe ambao wamekuwa waungaji mkono wake wakubwa, kwa mara ya kwanza kabisa walimtuhumu kiongozi huyo kuwa ni dikteta, matamshi ambayo yalitathminiwa na weledi wa mambo kama chachu ya kuimarisha harakati za upinzani dhidi ya Mugabe mwenye umri wa miaka 92.