Chukwuka: BRICS itahuisha uchumi na kupunguza ushawishi wa Magharibi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i121854-chukwuka_brics_itahuisha_uchumi_na_kupunguza_ushawishi_wa_magharibi
Kujiunga Nigeria na jumuiya ya BRICS kama nchi mshirika ni hatua kubwa kuelekea ufufuaji wa uchumi na kupunguza ushawishi wa Magharibi.
(last modified 2025-01-25T02:56:18+00:00 )
Jan 25, 2025 02:56 UTC
  • Chukwuka: BRICS itahuisha uchumi na kupunguza ushawishi wa Magharibi

Kujiunga Nigeria na jumuiya ya BRICS kama nchi mshirika ni hatua kubwa kuelekea ufufuaji wa uchumi na kupunguza ushawishi wa Magharibi.

Hayo yamesemwa na Emmanuel Chukwuka Johnson, Mwenyekiti wa Baraza la Ushauri la Biashara na Uwekezaji la Nigeria-Russia, katika mahojiano maalumu na Russia Today na kuongeza kuwa, "BRICS inatoa fursa yenye kutia matumaini katika kukabiliana na changamoto za muda mrefu za kiuchumi za Nigeria."

Chukwuka Johnson ameeleza bayana kuwa, "BRICS ni klabu ya marafiki wa kweli, klabu ya washirika" inayotaka "kukabiliana na ushawishi wa Magharibi; na Nigeria ni mwathirika wa kile ambacho sera za Magharibi zimekuwa zikizalisha. Hivyo BRICS inatoa fursa kwa Nigeria. Ili kufufua uchumi wetu, BRICS inatoa suluhisho."

Alipoulizwa jinsi mataifa ya Kiafrika yanaweza kutumia fursa zilizopo za BRICS, Chukwuka Johnson alisisitizia haja ya kuongeza viwango vya biashara na mabadilishano, na vile vile "kufanya miamala ya biashara kwa kutumia sarafu zao wenyewe, bila kutegemea sarafu pekee ambayo inaweza kutumika kama silaha."

Emmanuel Chukwuka Johnson, Mwenyekiti wa Baraza la Ushauri la Biashara na Uwekezaji la Nigeria-Russia

Wanachama wa BRICS wanakusudia kukabiliana na udhibiti wa sarafu ya dola ya Marekani juu ya uchumi wa dunia, na kushirikishwa mataifa yanayoibukia kiuchumi katika usimamizi wa uchumi wa dunia.

Nchi za BRICS zinazozalisha zaidi ya robo ya utajiri wa dunia na zinaunda asilimia 42 ya jamii ya watu wote duniani, zinataka kuwepo uwiano wa kisiasa na kiuchumi hasa mkabala wa Marekani na nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya.