Makumi ya wanajeshi wa Nigeria wauawa katika shambulio la kigaidi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i121940-makumi_ya_wanajeshi_wa_nigeria_wauawa_katika_shambulio_la_kigaidi
Watu wanaoshukiwa kuwa magaidi wamewaua wanajeshi 20 wa Nigeria, akiwemo kkamanda wa ngazi ya juu, baada ya kushambulia kambi moja ya jeshi katika jimbo la Borno la kaskazini mashariki.
(last modified 2025-01-27T02:25:56+00:00 )
Jan 27, 2025 02:25 UTC
  • Makumi ya wanajeshi wa Nigeria wauawa katika shambulio la kigaidi

Watu wanaoshukiwa kuwa magaidi wamewaua wanajeshi 20 wa Nigeria, akiwemo kkamanda wa ngazi ya juu, baada ya kushambulia kambi moja ya jeshi katika jimbo la Borno la kaskazini mashariki.

Wapiganaji wa kundi la Boko Haram na wanamgambo wa ISWAP wamekuwa wakiendesha operesheni zao zaidi mjini Borno, wakilenga vikosi vya usalama na raia, katika harakati hiyo ya kuua na kuwafukuza makumi ya maelfu ya watu.

Duru za kiusalama ziliarifu jana Jumapili kuwa, wanachama wa genge la kigaidi la ISWAP waliowasili wakiwa juu ya malori huku wakiwa wamejizatiti kwa bunduki, walishambulia kambi ya Kikosi cha 149 cha jeshi katika mji wa Malam-Fatori, mpakani na Niger.

Mmoja wa wanajeshi walionusurika katika shambulio hilo ameambia shirika la habari la Reuters kwa njia ya simu kwamba, lilikuwa shambulizi la kushtukizwa, ambapo wanamgambo hao "wakimimina risasi kila mahali".

“Tulijaribu sana kuzima mashambulizi hayo na baada ya zaidi ya saa tatu za makabiliano ya risasi, walituzidi nguvu na kumuua afisa wetu mkuu, Luteni Kanali,” amesema askari huyo huku akikataa kutajwa jina kwa sababu hana mamlaka ya kuzungumza na vyombo vya habari.

Mbali na kusakamwa na matatizo ya kkiuchumi, Nigeria inakabiliana pia na changamoto za kiusalama zinazosababishwa na magenge ya kigaidi hasa ISWAP na Boko Haram.