Waasi wa M23 wakaribia kudhibiti kikamilifu mji muhimu wa Goma DRC
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i122062-waasi_wa_m23_wakaribia_kudhibiti_kikamilifu_mji_muhimu_wa_goma_drc
Waasi wa M23 wanaonekana kukaribia kuudhibiti mji muhimu wa Goma mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kufuatia ripoti kwamba wameuteka uwanja wake wa ndege.
(last modified 2025-01-29T09:16:04+00:00 )
Jan 29, 2025 09:16 UTC
  • Waasi wa M23 wakaribia kudhibiti kikamilifu mji muhimu wa Goma DRC

Waasi wa M23 wanaonekana kukaribia kuudhibiti mji muhimu wa Goma mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kufuatia ripoti kwamba wameuteka uwanja wake wa ndege.

Serikali ya Congo imesisitiza kuwa bado ina udhibiti huku mapigano katika baadhi ya maeneo ya mji huo yakiendelea. Maghala yenye chakula na vifaa vya matibabu yameporwa, mashirika ya misaada yanasema.

Mapigano kati ya waasi wa M23 na jeshi na washirika wake yamesababisha hospitali kuzidiwa na majeruhi na miili iliyolala mitaani, kulingana na Umoja wa Mataifa.

Kuongezeka kwa hasira kuhusu mashambulizi ya waasi kulisababisha waandamanaji kulenga balozi za kigeni katika mji mkuu, Kinshasa. Wito wa mazungumzo ya amani kukomesha mapigano unazidi kuongezeka.

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), Felix Tshisekedi, amekataa kuhudhuria mkutano wa dharura wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ulioitishwa na Rais William Ruto wa Kenya kuhusu mgogoro wa kiusalama mashariki mwa jimbo la Kivu kaskazini.

Rais Ruto, ambaye ni mwenyekiti wa EAC, aliitisha mkutano wa dharura tarehe 29 Januari kwa ajili ya kushughulikia mzozo unaoongezeka mashariki mwa mji muhimu wa Goma mashariki mwa DRC.

Mapigano makali yanaendele kati ya wapiganaji wa M23 na wanajeshi wa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC katika mji wa Goma mashariki mwa nchi hiyo huku yakiacha maiti nyingi zikiwa zimezagaa mitaani, na hospitali nazo zikielemewa na ongezeko la majeruhi.