Libya yakomboa wahamiaji 263 waliokuwa wanashikiliwa na wahalifu wanaotaka kikomboleo
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Libya imetangaza habari ya kukombolewa wahamiaji 263 waliokuwa wametekwa na genge la wahalifu katika mji wa mashariki wa Jalu kwa ajili ya kupata kikomboleo.
Ofisi hiyo imesema katika taarifa iliyochapishwa jana kwenye ukurasa wake rasmi wa Facebook kwamba, maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Jinai walichunguza taarifa ya kutekwa wahamiaji haramu 263 ili kuzilazimisha familia zao kulipa fedha za kuwakomboa watu wao na kwamba maafisa hao wamefanikiwa kukomboa watu hao kutoka mikononi mwa wahalifu hao.
"Wanachama wawili wa genge la uhalifu wametiwa mbaroni huku msako ukiendelea wa kuwasaka wanachama waliobakia wa genge hilo," imesema taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wahamiaji hao, ambao ni raia wa Somalia na Eritrea, waliteswa kikatili na genge hilo ambalo lilitaka kulipwa dola 17,000 za Kimarekani ili wawaachilie huru watu hao.
Taarifa hiyo pia imesema: "Genge hilo lilikuwa linajihusisha na biashara haramu ya binadamu na operesheni za uhamiaji haramu kutoka Libya. Aidha lilikuwa linafanya mateso, unyanyasaji wa kibinadamu na kuwafunga wahamiaji waliokuwa wanawateka nyara."
Tangu ulipoangushwa utawala wa kiongozi wa zamani Muammar Gaddafi mwaka 2011, wahamiaji haramu wengi wao wakiwa ni Waafrika wa nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara, wanatumia Bahari ya Mediterania kujaribu kuvuka bahari hiyo yenye mawimbi makubwa kuelekea Ulaya kutokea Libya.
Lakini tamaa hizo za alinacha mara nyingi huishia wahamiaji hao kuzama baharini au kuishia mikononi mwa magenge kama hayo hatari ya magendo ya binadamu, kuteswa, kunyanyaswa na kupigwa mnada masokoni kama bidhaa.