Rais Tshisekedi aapa kuendesha vita 'vikali' vya kuwakomesha waasi wa M23
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i122098-rais_tshisekedi_aapa_kuendesha_vita_'vikali'_vya_kuwakomesha_waasi_wa_m23
Rais Félix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ameapa kurejesha mamlaka ya serikali mashariki mwa nchi, ambako waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda wameuteka mji wa Goma na wanaripotiwa kuelekea kusini kuchukua maeneo zaidi.
(last modified 2025-01-30T08:45:15+00:00 )
Jan 30, 2025 08:45 UTC
  • Rais Tshisekedi aapa kuendesha vita 'vikali' vya kuwakomesha waasi wa M23

Rais Félix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ameapa kurejesha mamlaka ya serikali mashariki mwa nchi, ambako waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda wameuteka mji wa Goma na wanaripotiwa kuelekea kusini kuchukua maeneo zaidi.

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Felix Tshisekedi amesisitiza kuwa wanajeshi wake wanapambana vikali kurejesha maeneo yaliyotwaliwa na waasi wa kundi la M23 linaloungwa mkono na Rwanda.

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Felix Tshisekedi, amesema jeshi lake linaendesha operesheni kali dhidi ya wapiganaji wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda, baada ya kundi hilo kuteka maeneo mapya mashariki mwa nchi.

Ameonya kuwa mashambulizi ya M23 yanaweza kuchochea mzozo mkubwa zaidi wa kikanda, huku hali ya kibinadamu ikizidi kuzorota.

Rais Tshisekedi ameikosoa jamii ya kimataifa kwa "kutochukua hatua" na kwa kutofanya juhudi za kutosha kufuatia mzozo wa usalama unaozidi kuongezeka.

Wakuu wa mataifa ya Afrika Mashariki waliokutana kwa njia ya vidio jana usiku, wametoa wito ws kusitisha mara moja vita hivyo, na kuitaka serikali ya Kinshasa kufanya mazungumzo na waasi hao.

Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, mapigano hayo yamewalazimu takriban watu 500,000 kukimbia makazi, na kuzidisha hali mbaya ya kibinadamu.

Kabla ya hapo, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) iliripoti kutokea ghasia na uporaji wa maghala ya misaada ya kibinadamu huko Goma na kuathiri uwezo wa wafanyakazi wa kimataifa katika kusambaza misaada hiyo kwa watu walioko hatarini zaidi.