Vyanzo vya jeshi Sudan: Dagalo anatekeleza Mpango B katika vita vya ndani
Vyanzo vya kijeshi katika Wizara ya Ulinzi ya Sudan vimefichua kwamba Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) hivi sasa vinatekeleza Mpango B (mpango mbadala) ambao kamanda wake, Mohamed Hamdan Dagalo "Hemedti", alitishia kuutekeleza baada ya kushindwa kunyakua madaraka.
Vyanzo hivyo vimeeleza kuwa RSF pamoja na viongozi wa mirengo kadhaa ya kisiasa, walipanga kutwaa madaraka Aprili 15, 2023 katika shambulio la haraka ambalo lisingechukua zaidi ya saa moja, lakini mpango huo haukufaulu.
Duru hizo ambazo hazikutaka kujatwa majina zimesema, Vikosi vya Msaada wa Haraka, vikisaidiwa na madola ya kikanda, vilipanga uvamizi wa haraka wa kijeshi baada ya kushindwa kwa "mapinduzi meupe." Ilikadiria kuwa vikosi vya jeshi havikuwa katika nafasi ya kukabiliana na wapiganaji wa RSF waliokuwa wamejizatiti Khartoum, kisha huo Darfur na majimbo ya Sennar na Al-Jazeera, wakijaribu kufika mashariki mwa Sudan na Port Sudan na kisha kuidhibiti nchi.
Ripoti zinasema, kwa sasa Vikosi vya Msaada wa Haraka vinatekeleza Mpango B, ambao Dagalo aliahidi kuutekeleza Oktoba mwaka jana baada ya vikosi vyake kupoteza eneo la kimkakati la Jebel Moya katika Jimbo la Sennar.
Mpango huo, kwa mujibu wa vyanzo vya kijeshi, unalenga kuharibu taasisi za huduma za umma kama vituo vya umeme na usafiri wa treni.
Mpango huo pia unalenga kueneza hali ya fazaa na kukata tamaa miongoni mwa raia, kulishutumu jeshi kuwa limeshindwa kulinda taasisi za huduma, na kufanya maisha ya watu kuwa magumu ili kuwalazimisha Wasudani kudai mazungumzo na Vikosi vya Msaada wa Haraka.