Mali: Tumemuangamiza kiongozi wa genge la kigaidi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i122126-mali_tumemuangamiza_kiongozi_wa_genge_la_kigaidi
Jeshi la Mali limetangaza kuwa limemuua kiongozi wa genge la kigaidi aliyekkuwa anaogoza vitendo vya kigaidi katikati mwa Mali.
(last modified 2025-01-31T02:59:11+00:00 )
Jan 31, 2025 02:59 UTC
  • Mali: Tumemuangamiza kiongozi wa genge la kigaidi

Jeshi la Mali limetangaza kuwa limemuua kiongozi wa genge la kigaidi aliyekkuwa anaogoza vitendo vya kigaidi katikati mwa Mali.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, magaidi wengine kadhaa nao wameangamizwa wakati wa operesheni kubwa iliyofanyika kote nchini Mali, siku za Jumanne na Jumatano.

Taarifa ya jeshi la Mali imeongeza kuwa: “Kiongozi huyo wa genge la kigaidi anajulikana kwa jina la Amadou Bolly. Alikuwa akiongoza vitendo vya kigaidi katika eneo la Kolongo. Ameuawa kwa kupigwa risasi pamoja na wenzake kadhaa katika operesheni iliyofanyika Jumanne kwenye maeneo ya Niaro, Nossombougou, Maninie, N'djibala, Boky Were na Kononga.”

“Bolly, ambaye alikuwa akisakwa kwa muda mrefu, anahusika na mauaji kadhaa, unyang'anyi na dhulma dhidi ya watu na raia wa kawaida,” imesema taarifa hiyo.

Vilevile jeshi la Mali limesema: Karibu magaidi 30, wakiwemo makamanda na wapiganaji kadhaa wameuawa huko Ghazaraghane, kaskazini mwa Mali, katika operesheni ya jeshi la Mali na wenzao kutoka Burkina Faso na Niger nchi tatu ambazo zinaunda jeshi la pamoja la Muungano wa Mataifa ya Sahel Afrika.

Tangu mwaka wa 2012, Mali imekuwa ikipambana na waasi wanaotaka kujitenga, uvamizi wa wanamgambo wenye silaha, magenge ya ukufurishaji na ghasia kati ya jamii mbalimbali. Matukio hayo yamesababisha maelfu ya watu kupoteza maisha na mamia ya maelfu kuyahama makazi yao.