Spika wa bunge la Algeria ataka kujinaishwa ukoloni wa Ufaransa nchini humo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i122128-spika_wa_bunge_la_algeria_ataka_kujinaishwa_ukoloni_wa_ufaransa_nchini_humo
Spika wa Bunge la Algeria, Ibrahim Boughali ametoa mwito wa kupasishwa sheria inayojinaisha ukoloni wa Ufaransa na kuutambua rasmi kuwa ni uhalifu. Mwito huo ni kiashiria tosha cha kuongezeka mvutano kati ya Algeria na mkoloni kizee wa Ulaya yaani Ufaransa.
(last modified 2025-01-31T02:59:41+00:00 )
Jan 31, 2025 02:59 UTC
  • Spika wa bunge la Algeria ataka kujinaishwa ukoloni wa Ufaransa nchini humo

Spika wa Bunge la Algeria, Ibrahim Boughali ametoa mwito wa kupasishwa sheria inayojinaisha ukoloni wa Ufaransa na kuutambua rasmi kuwa ni uhalifu. Mwito huo ni kiashiria tosha cha kuongezeka mvutano kati ya Algeria na mkoloni kizee wa Ulaya yaani Ufaransa.

Spika wa Bunge la Taifa la Algeria amelaani mashambulizi ya mara kwa mara ya Ufaransa dhidi ya matukufu ya Algeria na kusema: “Paris inakataa kukomesha tabia yake ya kuchafua sifa za Algeria." 

"Sasa, tunasema, wakati umefika wa kutanguliza mbele rasimu ya sheria inayotambua rasmi kwamba ukoloni wa Uaransa ni jinai na uhalifu. Inabidi rasimu hiyo ifuate mkondo wake wa asili." Amesema hayo katika mahojiano na televisheni binafsi ya Echorouk.

"Ninaamini kuwa mazingira sasa yanatulazimisha kupeleka mbele suala hili," akimaanisha kuongezeka mashambulizi ya maneno ya viongozi wa kisiasa wa Ufaransa dhidi ya Algeria.

Hii ni mara ya kwanza kwa kiongozi wa ngazi za juu kama huyo wa Algeria kutetea hadharani mpango wa kupitishwa sheria inayotambua utawala wa kikoloni wa miaka 132 wa Ufaransa nchini Algeria ulioanzia mwaka 1830 hadi 1962, kuwa ni jinai na uhalifu.

Spika Boughali ameeleza kuwa, sheria hiyo ilipendekezwa kwa mara ya kwanza mwaka wa 2006 kama jibu kwa muswada wa Ufaransa uliopuuza jinai na ukatili wote uliofanywa na wakoloni wa nchi hiyo ya Ulaya. Bunge la Ufaransa lilipasisha muswada huo na kuufanya kuwa sheria tarehe 13 Februari 2005.

Spika wa Bunge la Algeria amesema kuwa tayari rasimu ya sheria hiyo imefika ofisini kwake. Itafanyiwa marekebisho kidogo kabla ya kuwasilishwa rasmi kwa ajili ya mapitio, kujadiliwa na kupasishwa Bungeni.