Ethiopia kuongeza uwezo wa kuzalisha umeme maradufu ifikapo 2028
Serikali ya Ethiopia imetangaza kuwa ina mipango kabambe ya kuongeza uwezo wake wa kuzalisha nishati ya umeme hadi megawati 13,000 (MW) ifikapo mwaka 2028.
Hayo yamesemwa na Rais Taye Atske Selassie wa Ethiopia na kuongeza kuwa: "Nchi yetu (Ethiopia) inafanya kazi kwa bidii kupanua uwezo wake wa uzalishaji wa nishati mbadala ili kuweza kufikia malengo yake ya maendeleo kitaifa na kuzidi kuziunganisha nchi za ukanda huu na gridi ya umeme ya Ethiopia."
Selassie alitoa hakikisho hilo katika Mkutano wa Nishati wa Afrika uliofanyika jijini Dar es Salaam, Tanzania, mapema wiki hii. Hayo ni kwa mujibu wa ripoti ya jana ya Shirika la Fana Broadcasting.
Aidha amesema: Ethiopia, ambayo inasambaza umeme kwa nchi jirani za Djibouti, Kenya na Sudan, inashirikiana na nchi 14 za Afrika katika jitihada za kuimarisha ushirikiano wa nishati ya umeme kikanda.
Mwezi Novemba mwaka jana, Wizara ya Maji na Nishati ya Ethiopia ilisema kuwa, uwezo wa kuzalisha nishati nchini humo umeshapindukia MW 6,000, hasa kwa kutumia rasilimali nyingi za nishati mbadala za nchini humo.
Hivi karibuni Ethiopia ilitangaza pia mradi wa Njia Kuu ya Umeme ya Afrika Mashariki, mpango unaoendeshwa kwa pamoja na nchi za Ethiopia, Kenya na Tanzania, na umeshaanza kwa majaribio usambazaji wa umeme kutoka Kenya hadi Tanzania.