Zaidi ya watu milioni 67 wana uhaba wa chakula Pembe ya Afrika
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i122202-zaidi_ya_watu_milioni_67_wana_uhaba_wa_chakula_pembe_ya_afrika
Takriban watu milioni 67.4 wa eneo la Pembe ya Afrika hawana uhakika wa chakula. Hayo yametangazwa na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) na Jumuiya ya Maendeleo ya Kiserikali ya Afrika Mashariki (IGAD).
(last modified 2025-02-01T23:21:57+00:00 )
Feb 01, 2025 23:21 UTC
  • Zaidi ya watu milioni 67 wana uhaba wa chakula Pembe ya Afrika

Takriban watu milioni 67.4 wa eneo la Pembe ya Afrika hawana uhakika wa chakula. Hayo yametangazwa na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) na Jumuiya ya Maendeleo ya Kiserikali ya Afrika Mashariki (IGAD).

Taarifa ya mashirika hayo mawili imeongeza kuwa, hilo ni ongezeko la kutoka milioni 64.8 mwishoni mwa Novemba 2024 na kufikia milioni 67.4 hivi sasa. Ongezeko hilo limechangiwa na migogoro na majanga ya hali ya hewa katika ukanda huo.

Kati ya watu milioni 67.4, milioni 38 wanaishi kwenye nchi wanachama wa IGAD zikiwemo Djibouti, Ethiopia, Kenya, Somalia, Sudan Kusini, Sudan na Uganda. Wengine wako katika nchi nyingine zinazounda Pembe ya Afrika yaani Jamhuri ya Afrika ya Kati na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ambayo ina eneo kubwa la ardhi linalofika hadi katikati mwa Afrika.

Taasisi hizo mbili zimeongeza kwenye taarifa yao ya pamoja kwamba: "Migogoro inaendelea kuwa kichocheo kikuu cha matatizo ya chakula Afrika huku takriban watu milioni 38 katika eneo lote la IGAD wakiteseka kwa kiwango kikubwa cha uhaba wa chakula. Matatizo hayo yanachochea pia ukosefu wa usalama, uporaji, makundi ya waasi na vita visivyoisha."

Kwa mujibu wa mashirika hayo mawili, eneo la Pembe ya Afrika lina zaidi ya watu milioni 29 waliokimbia makazi yao kutokana na migogoro, hatari za kiusalama na majanga ya kimaumbile hasa katika nchi za Sudan na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.

Kwa upande wake, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) imebainisha kuwa, majanga ya mara kwa mara ya hali ya hewa na migogoro inazidisha umaskini na uhaba mkubwa wa chakula na utapiamlo katika eneo la Pembe ya Afrika.