DRC yataka Arsenal, Bayern Munich na PSG kufuta kandarasi zao na Rwanda
Mgogoro wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na Rwanda umeingia katika hatua mpya baada ya Kinshasa kuvitaka vilabu vya soka barani Ulaya vyenye kandarasi na serikali ya Kigali kusitisha kandarasi hizo.
Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imeziandikia timu za soka barani Ulaya zinazopata ufadhili kutoka serikali ya Rwanda kutopokea, 'Fedha zinazotokana na umwagikaji wa damu,' unaoendelea mashariki mwa DRC.
Kulingana na DRC, Waziri wake wa mambo ya kigeni Therese Kayikwamba Wagner ameziandikia klabu za Arsenal ya Uingereza, Paris Saint-Germain ya Ufaransa na Bayern Munich ya Ujerumani kusitisha ushirikiano wao wa ufadhili wa mauzo chini ya mpango wa, 'Visit Rwanda,' wakidai kwamba idadi kubwa ya wanajeshi wa Rwanda wanapigana na jeshi la FARDC huko Goma wakisaidiana na kundi la waasi la M23.
Katika barua yake kwa klabu ya Arsenal ya Uingereza Waziri Wagner amesema kwamba, 'Rwanda inastahili kulaumiwa kwa hatua zake ndani ya DRC kwani Umoja wa Mataifa umeripoti kwamba kikosi cha wanajeshi 4,000 kutoka Rwanda kiko ndani ya DRC na kinashikriki kwenye vita vinavyoendelea nchini humo.'
Na huku klabu hizo zikisubiriwa kufanya uamuzi kuhusu ombi hilo la serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na shutuma dhidi ya Rwanda, DRC imeendelea kuwasilisha hoja yake ya hali mbaya inayoshuhudiwa mashariki mwa nchi hiyo.