Burundi yaonya kuhusu kutokea vita vikubwa vya kikanda
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i122248-burundi_yaonya_kuhusu_kutokea_vita_vikubwa_vya_kikanda
Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye ameonya kuwa mzozo unaoongezeka mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo unaweza kuzusha vita vikubwa zaidi vya kikanda katika eneo la Maziwa Makuu.
(last modified 2025-02-02T23:56:15+00:00 )
Feb 02, 2025 23:56 UTC
  • Evariste Ndayishimiye
    Evariste Ndayishimiye

Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye ameonya kuwa mzozo unaoongezeka mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo unaweza kuzusha vita vikubwa zaidi vya kikanda katika eneo la Maziwa Makuu.

Rais Ndayishimiye wa Burundi ameitoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza na wanadiplomasia mjini Bujumbura huku video kadhaa zikisambaa kwenye mitandao ya kijamii.

Ndayishimiye alisema: "Ikiwa Mashariki mwa Kongo haitokuwa na amani, eneo hilo haliwezi kuwa na amani. Ikiwa itaendelea hivi, kuna hatari ya vita kuenea katika ukanda mzima." na kuongeza kuwa : "Kama Rwanda itaendelea kutaka kuchukua maeneo zaidi na najua vita vitafika hadi Burundi, hatutokubali na vita vitaenea kote na mjiandae kwa matokeo yake."

Burundi iliwatuma wanajeshi wake mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kama sehemu ya kikosi cha Jumuiya ya Afrika Mashariki ili kuliunga mkono jeshi la Kongo. Wanajeshi wa kikosi hicho cha EAC ispokuwa wanajeshi wa Burundi walishutumiwa na DRC pamoja na wakazi wa eneo hilo kwa kushirikiana na vikosi vinavyoipinga serikali ya Kinshasa.

Wanajeshi wa Burundi wamevisaidia vikosi vya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kuwadhibiti waasi wa M23 kuelekea mji wa Bukavu, huku wakifanikiwa pia kuchukua tena udhibiti wa maeneo yaliyokuwa yametekwa na waasi hao.

Mashambulizi ya waasi wanaoungwa mkono na Rwanda wa M23 yalionekana kudhibitiwa siku ya Jumamosi (01.02.2025) mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo baada ya jeshi la Kinshasa likisaidiwa na askari wa Burundi kupata mafanikio kadhaa kwenye uwanja wa vita. Hayo yameelezwa na vyanzo kadhaa ikiwa ni pamoja na asasi za kiraia na maafisa wa eneo hilo.