Jeshi la Sudan lasonga mbele kuelekea katikati ya Khartoum
Jeshi la Sudan lilitangaza jana, Jumatano, kuwa limepiga hatua kubwa za maendeleo katika mji mkuu, Khartoum, na kudhibiti kitongoji cha Al-Rumaila, makao makuu ya vifaa vya matibabu.
Duru za uwanjani zimeviambia vyombo vya habari kwamba vikosi vya jeshi la Sudan vimechukua udhibiti wa vitongoji vyote vya Al-Rumaila na Al-Sajana na eneo la viwanda magharibi mwa mji mkuu, Khartoum.
Vyanzo hivyo vimeeleza kuwa jeshi hilo sasa liko karibu na Mtaa wa Al-Ghaba unaoelekea katikati mwa Khartoum, ambako kuna wapiganaji wa Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF). Vimeongeza kwamba vikosi vya jeshi la vifaru vya Sudan vinapanga kujiunga na vitengo vya jeshi katika eneo la Al-Muqrin, ambapo vimejizatiti tangu Septemba mwaka jana, na katika makao makuu ya Kamandi Kuu katikati mwa jiji.
Siku chache zilizopita, Jeshi la Sudan lilitangaza kuwa limeudhibiti kikamilifu mji wa Khartoum Bahri, mojawapo ya maeneo makuu matatu ya mji mkuu wa nchi hiyo, Khartoum.
Taarifa ya jeshi la Sudan imesema, kwamba vikosi vyake vimedhibiti mhimili wa Al-Mak Bridge, kusini mwa Khartoum Bahri, na kwamba vinasonga mbele kusafisha eneo hilo.
Khartoum Bahri ni moja ya miji mitatu inayounda mji mkuu wa Sudan, pamoja na Omdurman na Khartoum.
Hapo awali jeshi la Sudan lilikuwa limedhibiti maeneo makubwa ya Omdurman.