Uganda yakanusha kuwatuma wanajeshi wa ziada mashariki ya DRC
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i122404-uganda_yakanusha_kuwatuma_wanajeshi_wa_ziada_mashariki_ya_drc
Jeshi la Uganda limekanusha rasmi madai kwamba limepeleka wanajeshi wake Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, ambapo vikosi vya Congo vinapigana na waasi wa M23.
(last modified 2025-02-06T23:08:43+00:00 )
Feb 06, 2025 23:08 UTC
  • Uganda yakanusha kuwatuma wanajeshi wa ziada mashariki ya DRC

Jeshi la Uganda limekanusha rasmi madai kwamba limepeleka wanajeshi wake Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, ambapo vikosi vya Congo vinapigana na waasi wa M23.

Awali iliripotiwa kwamba, Uganda imetuma wanajeshi zaidi ya 1,000 wa ziada huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ndani ya wiki moja iliyopita, karibu na eneo ambalo wanajeshi wa serikali ya Kinshasa wanapambana na waasi wa M23.

Vyanzo vya Umoja wa Mataifa viliripoti kuwa, hatua hiyo imeongeza idadi ya wanajeshi wa Uganda waliotumwa rasmi kuiunga mkono serikali ya Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Felix Tshisekedi, hadi karibu 5,000.

Licha ya kukanusha ripoti hiyo, Kampala imesisitiza maofisa ambao imewatuma nchini DRC ni sehemu ya walinda usalama wa oparesheni shujaa pekee.

Operesheni Shujaa imekuwa ikitekelezwa kwa ushirikiano wa wanajeshi wa DRC na wale wa Uganda katika vita dhidi ya waasi wa  ADF  wanaohusishwa na kundi la Islamic State tangu mwaka wa 2021.

Lengo la oparesheni shujaa ni kuwaondoa waasi wa ADF ambao wamekuwa wamekuwa wakitekeleza mashambulio mabaya kwa kipindi cha miaka 10.

Wakati huo huo, mji wa uchimbaji madini wa Nyabibwe, yapata kilomita 100 kutoka Bukavu, mji mkuu wa mkoa wa Kivu Kusini, umeangukia mikononi mwa waasi wenye silaha na wanajeshi wa Rwanda siku ya Jumatano, Februari 5.

Baada ya kuchukua Goma, mji mkuu wa mkoa jirani wa Kivu Kaskazini, Januari 27, M23 ilitangaza kwa upande mmoja usitishaji mapigano kwa sababu za kibinadamu ambao ulipaswa kuanza kutekelezwa tarehe 4 Februari.