Jeshi la Sudan laendelea kuyakomboa maeneo yanayoshikiliwa
Jeshi la Sudan limeendeleza mikakati yake ya kulikomboa eneo la katikati la mji mkuu Khartoum baada ya wiki ya mapambano inayolenga kuyakomboa maeneo mengi yanayodhibitiwa na wanamgambo wa RSF.
Ripoti zilizoifikia Radio Tehran zinasema, jeshi la Sudan limefanikiwa kuchukua udhibiti wa kambi muhimuu ya jeshi inayotumiwa kuidhibiti barabara kutoka katikati mwa Khartoum kuelekea Omdurman kuvuka mto Nile, mji ambao pamoja na Khartoum kaskazini, ni sehemu pana ya mji mkuu Khartoum.
Hata hivyo, msemaji wa wapiganaji wa RSF amesema taarifa za kusonga mbele wanajeshi wa Sudan ni za uongo.
Kwa upande wake jeshi la Sudan sambamba na kusisitiza mafanikio hayo limeeleza kuwa, jeshi linakaribia kulifikia lengo lake la kuungana na vikosi vinavyotokea jimbo la Al-Jazira, kusini mwa Khartoum.
Siku chache zilizopita, Jeshi la Sudan lilitangaza kuwa limeudhibiti kikamilifu mji wa Khartoum Bahri, mojawapo ya maeneo makuu matatu ya mji mkuu wa nchi hiyo, Khartoum.
Wakati huo huo, Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) limesema kuwa, idadi ya wakimbizi wa ndani (IDP) katika Pembe ya Afrika iliongezeka hadi milioni 20.75 kufikia mwishoni mwa mwaka uliopita wa 2024.
Shirika hilo la Umoja wa Mataifa lilisema hayo jana Jumanne katika ripoti iliyotolewa Nairobi, mji mkuu wa Kenya na kuongeza kuwa, idadi hiyo iliongezeka kutoka milioni 20.42 mwezi Oktoba 2024, hadi milioni 20.75 mwezi Disemba 2024, kutokana na kuongezeka kwa wakimbizi wa ndani nchini Sudan.