Rais Samia awataka viongozi wa kikanda kuupatia ufumbuzi mgogoro wa DRC
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i122478-rais_samia_awataka_viongozi_wa_kikanda_kuupatia_ufumbuzi_mgogoro_wa_drc
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ni mwenyeji wa mkutano wa kilele wa kikanda wa kutatua mzozo wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo amewataka viongozi wa kikkanda kuupatia ufumbuzi mgogoro wa nchi hiyo hharaka iwezekanavyo.
(last modified 2025-02-08T09:40:04+00:00 )
Feb 08, 2025 09:40 UTC
  • Rais Samia awataka viongozi wa kikanda kuupatia ufumbuzi mgogoro wa DRC

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ni mwenyeji wa mkutano wa kilele wa kikanda wa kutatua mzozo wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo amewataka viongozi wa kikkanda kuupatia ufumbuzi mgogoro wa nchi hiyo hharaka iwezekanavyo.

Mama Samia amewataka viongozi wa ukanda huo kutafuta suluhu la mzozo huo, huku akionya kuwa iwapo watashindwa, historia itawahukumu vikali.

Rais Samia Suluhu Hassan ameutaka Umoja wa Afrika kupitia Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) kuhakikisha kuwa mgogoro wa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) unapatiwa suluhisho la kudumu.

Akizungumza katika Mkutano wa Pamoja wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa EAC na SADC unaofanyika jijini Dar es Salaam kujadili hali ya usalama mashariki mwa DRC, Rais Samia amesisitiza kuwa Tanzania inaheshimu dhamira ya kulinda amani na usalama, si tu ndani ya kanda bali barani Afrika kwa ujumla.

Mkutano wa SADC na EAC Dar es Salaam Tanzania

 

Katika hotuba yake, Rais Samia ameeleza kwamba mgogoro wa DRC, taifa ambalo ni mwanachama wa EAC na SADC, umeendelea kwa muda mrefu na athari zake zimevuka mipaka na kuathiri mataifa jirani kwa namna mbalimbali, ikiwemo ongezeko la wakimbizi, kuporomoka kwa shughuli za kiuchumi, na kutishia usalama wa raia wasiokuwa na hatia.

Rais Samia amebainisha kuwa Tanzania itaendelea kushiriki kikamilifu katika juhudi za kidiplomasia ili kuhakikisha kuwa mgogoro wa DRC unapata suluhisho la kudumu. Amesisitiza kuwa ni muhimu kwa mataifa ya Afrika kusimamia utatuzi wa changamoto zao kwa misingi ya “suluhisho za Kiafrika kwa matatizo ya Afrika.”