UN: Mapigano yaendelea Kivu Kusini, watu wengi wahama makazi yao
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i122492-un_mapigano_yaendelea_kivu_kusini_watu_wengi_wahama_makazi_yao
Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, wakati vita vikipungua katika mji wa Goma unaokaliwa kwa mabavu na waasi ambao UN inasema wanaungwa mkono na Rwanda, maafisa wake wa huduma za kibinadamu wamesema kuwa, mapigano yamepamba moto katika jimbo la Kivu Kusini na kusababisha watu wengi kuhama makazi yao.
(last modified 2025-02-08T22:56:47+00:00 )
Feb 08, 2025 22:56 UTC
  • UN: Mapigano yaendelea Kivu Kusini, watu wengi wahama makazi yao

Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, wakati vita vikipungua katika mji wa Goma unaokaliwa kwa mabavu na waasi ambao UN inasema wanaungwa mkono na Rwanda, maafisa wake wa huduma za kibinadamu wamesema kuwa, mapigano yamepamba moto katika jimbo la Kivu Kusini na kusababisha watu wengi kuhama makazi yao.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) imesema kwenye ripoti yake kwamba, mripuko wa bomu huko Kivu Kusini ulijeruhi raia watatu juzi Ijumaa na kuharibu miundombinu ya umeme katika mji wa Nyabibwe, ulioko takriban kilomita 60 kaskazini mwa makao makuu ya jimbo hilo yaani Bukavu.

Mapigano yanayoendelea Kivu Kusini yanasababisha watu wengi kuyahama makazi yao na wengine kuuawa. Maelfu ya watu wako kwenye harakati za kukimbia ili kusalimisha maisha yao. Wengi wanakimbilia upande wa mji wa Bukavu ambao nao uko kwenye hatari ya kushambuliwa na waasi wa M23.

Maafisa wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa wamesema kuwa, wao na washirika wao hivi sasa wako kwenye zoezi la kutathmini hali ndani na karibu na mji wa Goma ambako mamia ya maelfu ya watu bado wako kwenye harakati za kukimbia.

OCHA imeripoti pia kwamba, wafanyakazi watatu wa shirika moja lisilo la kiserikali (NGO) waliuawa kwenye shambulio la bomu siku ya Jumatano katika jimbo la Kivu Kaskazini na kulazimisha kusitishwa msaada wa chakula na kilimo uliokuwa unasambazwa kwenye eneo hilo.

Kwa mujibu wa makadirio ya OCHA, karibu watu 33,000 wamesharejea katika vijiji vya Nyiragongo, kaskazini-mashariki mwa Goma.