Wanajeshi wa Ufaransa kuondoka Senegal mwishoni mwa 2025
(last modified Thu, 13 Feb 2025 10:30:47 GMT )
Feb 13, 2025 10:30 UTC
  • Wanajeshi wa Ufaransa kuondoka Senegal mwishoni mwa 2025

Ufaransa na Senegal zimeeleza kuwa zimeamua kuunda tume itakayoafanya maandalizi ya kuondoka wanajeshi wa Ufaransa katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi ifikapo mwisho mwa mwaka huu.

Taarifa ya pamoja ya nchi hizo imeeleza kuwa, Senegal na Ufaransa zimekusudia kufanya kazi kuelekea kuwa na ubia katika ulinzi na usalama unaozingatia vipaumbele vya kimkakati vya pande zote.

Rais Bassirou Diomaye Faye wa Senegal mwaka jana alisema anataka kusitisha uwepo wa wanajeshi wa Ufaransa nchini humo. "Karibuni hivi wanajeshi wa Ufaransa hawatakuwepo Senegal," Faye aliliambia gazeti la Le Monde mwezi Novemba mwaka jana ambapo alitilia mkazo umuhimu wa mamlaka ya kitaifa ya nchi. 

Maoni hayo ya Rais Faye wa Senegal yalikuwa ya kwanza kuwahi kutolewa na serikali ya nchi hiyo kuhusu suala la kuondoka Senegal wanajeshi wa Ufaransa.

Inafaa kuashiria hapa kuwa, jeshi la Ufaransa limeendelea kuwepo nchini Senegal tangu nchi hiyo ilipopata uhuru mwaka 1960, hususani katika uga wa mafunzo na kile kilichojulikana kama operesheni za usalama za kikanda.

Waziri Mkuu wa Senegal Ousmane Sonko mwezi Mei mwaka jana alikosoa uwepo wa wanajeshi wa Ufaransa nchini humo akisisitiza ulazima wa kuheshimiwa mamlaka ya kujitawala nchi hiyo.