Polisi ya Nigeria yakadhibisha kutoweka maelfu ya bunduki
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i122690-polisi_ya_nigeria_yakadhibisha_kutoweka_maelfu_ya_bunduki
Jeshi la Polisi la Nigeria limekanusha ripoti kwamba maelfu ya silaha zimetoweka kwenye maghala yake ya silaha na kuitaja rupoti hiyo kuwa ni ya kupotosha na isiyo sahihi.
(last modified 2025-02-13T11:20:31+00:00 )
Feb 13, 2025 11:20 UTC
  • Polisi ya Nigeria yakadhibisha kutoweka maelfu ya bunduki

Jeshi la Polisi la Nigeria limekanusha ripoti kwamba maelfu ya silaha zimetoweka kwenye maghala yake ya silaha na kuitaja rupoti hiyo kuwa ni ya kupotosha na isiyo sahihi.

Taarifa hiyo imetolewa kufuatia mkutano kati ya Kamati ya Seneti ya Nigeria ya Hesabu za Serikali na maafisa wakuu wa polisi ya nchi hiyo huku kukiwa na wasiwasi juu ya mashambulizi ya mara kwa mara ya makundi yenye silaha nchini humo.

Vyombo vya habari vya Nigeria vimearifu kuwa mkutano huo ulijadili suala la bunduki 178,459 zinazodaiwa kuptoweka, zikiwemo bunduki 88,078 aina ya  AK-47, kutoka kwenye orodha ya polisi iliyochapishwa kwa mara ya kwanza na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu wa Nigeria mwaka 2019.

Olumiyiwa Adejobi Msemaji wa Polisi ya Nigeria ameeleza kuwa hakuna idadi kubwa ya bunduki zilizokosekana kwenye maghala ya silaha ya polisi ya nchi hiyo. 

"Ni muhimu kutambua changamoto zinazowakabili polisi wakati wa machafuko ya wenyewe kwa wenyewe, ambapo askari polisi kadhaa waliuawa na silaha zao kuchukuliwa, na upotevu wa silaha umeshuhudiwa katika baadhi ya mashambulizi na uporaji wa vituo vya polisi," amesema Msemaji wa Polisi ya Nigeria.

Nigeria imekuwa ikikabiliana na ukosefu wa usalama katika miaka ya hivi karibuni, huku makundi ya kigaidi, wanamgambo wenye silaha  na magenge ya utekaji nyara yakiendesha mashambulizi makubwa katika maeneo mbalimbali nchini humo.