Mkutano wa kikanda kuhusu mapigano Kongo DR kufanyika leo Dar es Salaam
Tanzania leo Jumatatu, inatazamiwa kuwa mwenyeji wa mkutano wa kikanda, kufuatilia matukio ya nyanjani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ili kuchukua hatua zinazohitajika za kukabiliana na mgogoro huo.
Mkutano huo unahudhuriwa na nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Mkutano huu unafanyika siku mbili baada ya viongozi wa majeshi ya Afrika Mashariki kukutana mjini Nairobi na kutoa mapendekezo ya kukabiliana na mzozo wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Mkutano huo wa Wakuu wa Majeshi umekuja kama sehemu ya juhudi za kukabiliana na mzozo unaozidi kuongezeka mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Wakuu hao wa majeshi walijadili uwezekano wa kutekeleza maazimio ya vikao vya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika vilivyofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Veronica Nduva, ameeleza kuwa mkutano huo umeandaliwa kwa dharura ili kukabiliana na mabadiliko makubwa ya hali ya kibinadamu tangu kufanyika kwa Mkutano wa Dar es Salaam.
Amesema kuwa matukio ya hivi karibuni katika eneo hilo yanahitaji hatua za haraka na za dharura ili kukabiliana na mzozo huo.
Nduva amezungumzia changamoto zilizopo na kuelezea matumaini yake kuwa amani ya kudumu, usalama na utulivu vinaweza kupatikana kupitia juhudi zinazoendelea kushughulikia vyanzo vya migogoro.
Taarifa iliyotolewa na mkutano huo wa viongozi wa majeshi ilisema kuwa vuguvugu la M23 limepanua wigo wa operesheni zake huko Kivu Kusini, huku mapigano yakiendelea karibu na Kamanyola na kusonga mbele huko Lubero.