Mkutano wa G20 wafikia tamati bila mwafaka
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i123318-mkutano_wa_g20_wafikia_tamati_bila_mwafaka
Mkutano wa G20 uliokuwa ukifanyika nchini Afrika Kusini umemalizika bila ya washiriki wake kufikia mwafaka.
(last modified 2025-02-28T09:36:21+00:00 )
Feb 28, 2025 09:36 UTC
  • Mkutano wa G20 wafikia tamati bila mwafaka

Mkutano wa G20 uliokuwa ukifanyika nchini Afrika Kusini umemalizika bila ya washiriki wake kufikia mwafaka.

Afrika Kusini imesikitishwa na hatua ya kumalizika kwa mkutano wa G20 kuhusu uchumi wa dunia bila kupatikana mwafaka baada ya maafisa wa ngazi za juu kutoka nchi kadhaa kukwepa na wajumbe wengine kujiweka mbali na masuala ya kufadhili mabadiliko ya tabianchi.

Mkutano wa siku mbili wa G20 uliokutanisha mawaziri wa fedha na benki kuu mjini Cape Town Afrika Kusini ulishindwa pia kutoa taarifa ya pamoja.

Hata hivyo "taarifa fupi ya mwenyekiti" iliyotolewa na mwenyeji wa mkutano huo ilisema washiriki "walisisitiza kupinga sera ya kiuchumi inayozuia uagizaji bidhaa kutoka nje.

Muhtasari huo uliongeza kuwa, waliunga mkono mfumo wa biashara wa kimataifa unaozingatia kanuni, usio na ubaguzi, wa haki, shirikishi, endelevu na wa wazi," wakitumia maneno ambayo utawala wa Trump tayari umepinga vikali.

Afrika Kusini ilikuwa na matumaini ya kutumia mkutano huu wa G20 kuwa jukwaa la kushinikiza nchi tajiri kuongeza nguvu zaidi katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kusaidia zaidi nchi maskini katika mabadiliko ya kuelekea matumizi ya nishati safi na kufanya mageuzi katika mfumo wa kifedha unaopendelea uwekezaji wa kibenki kwa kukopesha mataifa maskini.

Lakini mazungumzo yaligubikwa na kukosekana kwa wadau muhimu wa fedha - kama vile Marekani, China, India na Japan - na kupunguzwa kwa misaada ya kigeni kutoka kwa taifa lenye uchumi mkubwa kama Marekani na Uingereza, huku kukiwa na hali ya ongezeko la mivutano ya kisiasa duniani.