Je, Afrika Kusini itasalimu amri mbele ya ubabe wa Trump?
Kwa kuendelea msimamo wa kuingilia kati wa Rais Donald Trump wa Marekani katika masuala ya ndani ya Afrika Kusini, serikali ya Pretoria imetangaza kuwa haitajiingiza katika diplomasia isiyo na tija ya "kupiga kelele kupitia vipaza sauti" na Marekani.
Serikali ya Afrika Kusini imeeleza kuwa Donald Trump ana uelewa usio sahihi kuhusu sheria mpya ya ardhi nchini humo. Sheria hii inaruhusu kuchukuliwa ardhi bila fidia katika baadhi ya hali.
Serikali ya Afrika Kusini imesisitiza kuwa uhusiano kati ya nchi hiyo na Marekani unapaswa kujengwa juu ya heshima ya pande zote, huku Pretoria ikiendelea kujitolea kuimarisha mahusiano ya kibiashara, kisiasa, na kidiplomasia kwa manufaa ya pande zote mbili.
Msimamo huu wa serikali ya Afrika Kusini umetolewa baada ya Trump kudai tena kupitia mitandao ya kijamii kuwa serikali ya Pretoria inawanyang’anya ardhi wazungu. Trump pia amedai kuwa Marekani iko tayari kuwapa uraia wakulima wazungu wa Afrika Kusini wanaopoteza ardhi zao. Hata hivyo, madai ya Trump kuhusu wasiwasi wake juu ya kuchukuliwa ardhi kutoka kwa wakulima wazungu yanaonekana kama kisingizio tu cha kuishinikiza Afrika Kusini. Viongozi wa Pretoria wameeleza kuwa madai hayo ni njama za Trump za kukata misaada kwa Afrika Kusini na kuishinikiza nchi hiyo. Sababu halisi ya hasira ya Trump dhidi ya Afrika Kusini ni hatua za kisheria zilizochukuliwa na serikali ya Pretoria dhidi ya uhalifu wa utawala wa Kizayuni wa Israel.
Afrika Kusini imesisitiza kuwa, licha ya vitisho vya serikali ya Marekani, haitaondoa kesi yake dhidi ya Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ).
Afrika Kusini ni moja ya nchi muhimu na zenye ushawishi mkubwa barani Afrika katika uwanja wa kisiasa na kimataifa. Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, imechukua msimamo mkali dhidi ya Israel na kuwasilisha mashtaka katika ICJ, hatua iliyosaidia kuhamasisha mataifa mengine duniani kufungua kesi dhidi ya Israel kutokana na mauaji yake ya kimbari dhidi ya Wapalestina. Kwa hakika, Afrika Kusini ilikuwa nchi ya kwanza mnamo Desemba 2023 kuwasilisha rasmi malalamiko dhidi ya Israel katika ICJ kuhusu jinai za utawala huo wa Kizayuni huko Gaza.
Sasa, huku Donald Trump akianza kuhudumia muhula wake mpya wa urais, anatumia madai ya wazungu kupokonywa ardhi kama kisingizio cha kuiwekea Afrika Kusini mashinikizo ya moja kwa moja na yasiyo ya moja kwa moja. Madai haya yanakuja licha ya ukweli kwamba, miaka mingi baada ya kumalizika kwa utawala wa ubaguzi wa rangi (Apartheid), bado sehemu kubwa ya ardhi ya Afrika Kusini inamilikiwa na wazungu. Tangu kumalizika mfumo wa Apartheid mwaka 1994, serikali mbalimbali za Afrika Kusini zimejaribu kupunguza ukosefu wa usawa wa kihistoria kwa kutekeleza sera za mageuzi ya ardhi.

Hata hivyo, wazungu ambao ni karibu asilimia 9 tu ya idadi ya watu wa Afrika Kusini, wanamiliki zaidi ya asilimia 72 ya ardhi za kilimo binafsi. Kwa sababu hiyo, mwanzoni mwa mwaka 2025, serikali ya Rais Cyril Ramaphosa ilipitisha sheria inayoruhusu serikali kutaifisha ardhi isiyotumika au inayofaa kwa manufaa ya umma bila malipo ya fidia katika hali maalum. Lengo la sheria hiyo ni kuharakisha mageuzi ya ardhi na kusambaza ardhi kwa haki zaidi.
Kwa kutekelezwa sheria hii, suala la kulinda maslahi ya wazungu wa Afrika Kusini limekuwa mojawapo ya visingizio vya Marekani vya kuiwekea mashinikizi serikali ya Pretoria. Elon Musk, mshauri wa Trump ambaye pia alizaliwa Afrika Kusini, bila kutoa ushahidi wowote, ameituhumu nchi hiyo kuwa na "sheria za umiliki wa ardhi zilizo wazi kibaguzi" na kudai kuwa wazungu ndio waathirika wa sera hizo.
Kwa hakika, Trump anajaribu kupotosha ukweli kuhusu suala hili na kuitishia Afrika Kusini kwa vitisho vya kukata misaada ili kuilazimisha ifuate matakwa ya Washington. Jambo kuu analolenga ni kuhakikisha kuwa Afrika Kusini inaondoa kesi yake dhidi ya utawala wa kibaguzi wa Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki.
Ronald Lamola, Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini, amesisitiza kuwa kusimamia misingi ya haki mara nyingine huleta madhara, lakini Afrika Kusini itaendelea kusimama imara kwa sababu suala hili ni muhimu kwa dunia na kwa utawala wa sheria.
Julius Malema, kiongozi wa chama cha Mapambano ya Uhuru wa Kiuchumi (EFF), amemwita Trump kuwa ni mwongo na mgonjwa, akisema: "Achana na Afrika Kusini, hatukuogopi."
Licha ya juhudi za Marekani za kulazimisha mataifa ya Afrika yafuate matakwa yake, Afrika Kusini imeendelea kushikilia msimamo wake wa kuunga mkono haki za Wapalestina na kuhifadhi mamlaka yake. Rais Cyril Ramaphosa amesisitiza kuwa nchi yake haitasalimu amri mbele ya ubabe wa Marekani.