Mripuko wa homa ya uti wa mgongo waua makumi Nigeria
(last modified Wed, 12 Mar 2025 07:05:01 GMT )
Mar 12, 2025 07:05 UTC
  • Mripuko wa homa ya uti wa mgongo waua makumi Nigeria

Watu wasiopungua 26 wameaga dunia kutokana na mripuko wa ugonjwa wa uti wa mgongo (Meningitis) katika Jimbo la Kebbi kaskazini magharibi mwa Nigeria.

Musa Ismaila, Kamishna wa Afya huko Kebbi, ameviambia vyombo vya habari katika makao makuu ya jimbo hilo, Birnin Kebbi kwamba, mripuko huo uliotangazwa mwishoni mwa Januari, ulizidi kuwa mbaya wiki iliyopita huku kesi zinazoshukiwa kuwa za maradhi hayo zikiongezeka ghafla.

Ismaila amebainisha kuwa, "Jumla ya kesi 248 zinazoshukiwa zimerekodiwa. Tunakabiliwa na hali mbaya ya mripuko na idadi kubwa ya kesi zenye dalili kama vile homa, maumivu makali ya kichwa, kukakamaa shingo, tumbo kuuma, kutapika, kuharisha na kuathiriwa na mwanga." 

Afisa huyo wa afya jimboni Kebbi amesema dawa na vifaa vingine vya matibabu vimesambazwa katika maeneo ya serikali za mitaa yaliyoathiriwa, na serikali ya jimbo inajitahidi kudhibiti hali hiyo.

Kwa mujibu wa Kituo cha Kudhibiti Magonjwa nchini Nigeria (NCDC), homa ya uti wa mgongo huua makumi au baadhi ya nyakati mamia ya watu hasa watoto kila mwaka. Ikumbukwe kuwa, watu 1,100 walipoteza maisha kutoka na mripuko mbaya zaidi wa ugonjwa huo katika nchi za Nigeria na Niger mwaka 2015, ambapo kesi elfu 10 ziliripotiwa.

Meningitis au homa ya uti wa mgongo ni ugonjwa unaosababishwa na virusi au bakteria, ambapo tishu zinazozunguka ubongo na uti wa mgongo wa muathiriwa huungua na kudhoofika.