Lassa yaua watu 118 Nigeria ndani ya miezi mitatu
(last modified Tue, 01 Apr 2025 10:35:59 GMT )
Apr 01, 2025 10:35 UTC
  • Lassa yaua watu 118 Nigeria ndani ya miezi mitatu

Homa ya Lassa imeua watu 118 nchini Nigeria katika kipindi cha miezi mitatu ya kwanza ya mwaka huu. Hayo yamesemwa na Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa cha nchi hiyo ya Afrika Magharibi (NCDC).

Virusi hivyo vinavyobebwa na panya na ambavyo vilitambulika kwa mara ya kwanza mwaka wa 1969 katika jimbo la kaskazini mashariki la Borno, vimeua maelfu ya watu tangu wakati huo, haswa katika maeneo ya vijijini kutokana na utunzaji usiofaa wa chakula.

Mkurugenzi Mkuu wa NCDC, Jide Idris amesema katika taarifa yake kuwa: Katika kipindi cha Januari-Machi, jumla ya kesi 645 za homa ya Lassa zilithibitishwa huku vifo 118 vikisajiliwa, hicho kikiwa ni kiwango cha vifo cha 18.3%. Nigeria imekuwa ikirekodi wastani wa vifo 100 kutokana na homa ya Lassa katika kila robo moja ya mwaka katika miaka ya hivi karibuni.

Idris amesema miongoni mwa kesi za hivi punde, zaidi ya wahudumu 20 wa afya waliambukizwa homa ya Lassa katika majimbo matano kati ya 33 yaliyoathiriwa nchini humo.

Licha ya miaka mingi ya kampeni ya kuzuia ugonjwa huo, lakini hakujawa na maboresho makubwa katika usafi wa mazingira miongoni mwa Wanigeria maskini wa vijijini; usafi ambao unaweza kuzuia panya hao kufikia makazi ya watu, chakula na vyombo vya jikoni.

Ugonjwa wa homa ya Lassa kwa kawaida huenezwa kwa kugusana na panya walioambukizwa, chakula kilichochafuliwa, au wahudumu wa afya ambao hukutana na wagonjwa walioambukizwa. Mgonjwa anaweza kudhihirisha dalili kuanzia kuwa na homa ya wastani hadi kali ikiwa ni pamoja na homa, maumivu ya kichwa na ya misuli.