Kagame azihutubu nchi zinazoiwekea Rwanda vikwazo: Nendeni kuzimu
(last modified Tue, 08 Apr 2025 06:55:28 GMT )
Apr 08, 2025 06:55 UTC
  • Kagame azihutubu nchi zinazoiwekea Rwanda vikwazo: Nendeni kuzimu

Rais Paul Kagame wa Rwanda amezikosoa vikali nchi ambazo hivi karibuni zilitangaza kuiwekea Kigali vikwazo kutokana na mgogoro wa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Akihutubia hadhira katika mkutano wa kila mwaka wa kumbukizi ya mauaji ya kimbari ya Rwanda ya 1994 jana Jumatatu, Kagame alizikosoa vikali nchi hizo hasa za Magharibi kwa kuiwekea vikwazo nchi yake kwa kisingizio cha vita vya mashariki ya Kongo DR.

Kagame amesema, "Wanakuja (katika nchi yako), kisha wanakwambia, tutakuwekea vikwazo. Nini? Nendeneni kuzimu!"

Pasi na kutaja nchi yoyote, Kagame ameendelea kusema: Mna matatizo yenu mnapasa kuyashughulikia, niachieni ya kwangu.

Haya yanajiri wiki chache baada ya Umoja wa Ulaya kuwawekea vikwazo makamanda wa jeshi la Rwanda, mwezi mmoja baada ya Washington kutangaza vikwazo dhidi ya Waziri katika serikali ya Kagame.

DRC na nchi za Magharibi zinaituhumu  Rwanda kwa kuunga mkono waasi wa M23 ambao tangu Januari wameteka miji ya Bukavu na Goma ya eneo lenye utajiri wa madini mashariki mwa DRC. Rwanda imekanusha madai hayo.

Waasi wa M23; Rwanda inakadhibisha kuliunga mkono kundi hilo

Mwishoni mwa mwezi uliopita, serikali ya Rwanda iliyapiga marufuku mashirika yote ya kimataifa na ya kitaifa yasiyo ya kiserikali (NGOs) na mashirika yanayofanya kazi nchini humo kushirikiana na serikali ya Ubelgiji na mashirika yake tanzu.

Kabla ya hapo, Ubelgiji ilijibu hatua ya Rwanda ya kukata uhusiano wake wa kidiplomasia na nchi hiyo ya Ulaya na kuwafukuza wanadiplomasia wa Rwanda nchini Ubelgiji.