Katibu Mkuu wa Hilali Nyekundu Sudan: Vita haviheshimu chochote
Huku vita vya ndani huko Sudan vikiingia katika mwaka wa tatu, Mkuu wa Shirika la Hilali Nyekundu la Sudan (Hilali Nyekundu) SRCS ametahadharisha kuhusu kuongezeka hatari zinazowakabili wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu katika mazingira magumu wanayofanyia kazi wakati wakitoa huduma kwa mamilioni ya watu walioathiriwa na vita.
Aida al Sayed Abdullah Katibu Mkuu wa Shirika la Hilali Nyekundu la Sudan amesisitiza kuhusu uhakika wa hali ya hatari wanayopitia kila siku wafanyakazi wa kujitolea na wengine wanaotoa huduma katika hali ya mchafukoge na uharibifu mkubwa inayoendelea kushuhudiwa huko Sudan.
"Ni vigumu sana kueleza kuwa tuna bima ya kuwalinda wafanyakazi hasa wale wa kujitolea kwa sababu vita vya Sudan haviheshimu kitu chochote," ameeleza Katibu Mkuu wa Shirika la Hilali Nyekundu la Sudan.
Jeshi la Sudan linapigana na wanamgambo wa RSF tangu Aprili mwaka juzi kwa ajili ya kuidhibiti nchi hiyo huku maelfu ya watu wakiwa wameuawa na wengine wengi kujeruhiwa katika mapigano hayo.