UN: Theluthi moja ya Wasudani ni wakimbizi, hali ya wanaokimbia kambi za Darfur ni janga tupu
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) limefichua kuwa mtu mmoja kati ya watatu nchini Sudan amelazimika kuwa mkimbizi, huku mamia ya watu wanaokimbia kambi za Darfur wakikabiliwa na hali mbaya kufuatia mashambulizi ya Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF).
Adam Rijal, msemaji wa Ofisi ya Uratibu wa UNHCR huko Darfur, ameripoti kwamba idadi kubwa ya watu waliokimbia makazi yao kutoka El Fasher na kambi za Zamzam na Abu Shouk wanaendelea kumiminika katika mji wa Tawila, magharibi mwa El Fasher.
Rijal amesema kwamba katika kipindi cha wiki mbili zilizopita tu takriban wakimbizi 400,000 wamewasili katika eneo hilo mbali na maelfu zaidi ambao wamekimbia makazi yao tangu kuongezeka kwa mapigano kati ya jeshi la Sudan na Vikosi vya Msaada wa Haraka, Mei mwaka jana.
Eneo la Tawila linadhibitiwa na Harakati ya Ukombozi wa Sudan inaloongozwa na Abdul Wahid Muhammad Nur na hivi karibuni limekuwa makimbilio ya makumi ya maelfu ya wakimbizi wa ndani (IDPs) wanaokimbia machafuko yanazozidi kuongezeka huko Darfur Kaskazini.
Kwa upande wake, Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka limeeleza hali katika kambi ya Tawila kuwa ni janga, huku watu waliokimbia makazi yao wakisumbuliwa na uhaba mkubwa wa maji, chakula na huduma za afya.
Mwakilishi wa shirika hilo, Thibaut Hendler, ameviambia vyombo vya habari kwamba: "Hakuna chanzo cha maji, hakuna vyoo wala chakula katika eneo ambalo lilikuwa tupu wiki moja iliyopita na sasa limejaa familia zilizokata tamaa."