Rais wa Kenya aelekea China baada ya Marekani kuongeza ushuru
Ziara ya siku tano ya Rais wa Kenya William Ruto nchini China inayoanza Jumanne imetajwa kuwa hatua muhimu katika mwelekeo wa kidiplomasia na kiuchumi wa Kenya, huku akilenga kukabiliana na hatua mpya zilizochukuliwa dhidi ya nchi hiyo na Marekani.
Wakati washirika wa jadi kutoka nchi za Magharibi hasa Marekani wakipunguza misaada ya kigeni na kuchukua hatua za kibiashara za kujilinda, Kenya imeonyesha nia ya kuimarisha ushirikiano wa kimkakati na China ili kufanikisha ajenda yake ya maendeleo.
Ziara ya Ruto inasisitiza dhamira ya Kenya kuimarisha ushirikiano wa pande mbili katika maeneo muhimu kama vile nishati, usafiri, teknolojia na kilimo, kwa mujibu wa maafisa wa serikali na wachambuzi.
Kwa mujibu wa gazeti la China Daily, ziara hiyo inafanyika katika muktadha wa vita vya kibiashara vinavyozidi kushadidi kati ya Washington na Beijing, ambavyo vimesababisha ushuru kuongezeka mara kadhaa baina ya mataifa hayo mawili, hali iliyovuruga minyororo ya usambazaji duniani na kuathiri uchumi wa Kenya unaotegemea mauzo ya nje.
Utawala wa Trump haukuisamehe Kenya licha ya kuwa mshirika wa muda mrefu, baada ya kuiwekea ushuru wa asilimia 10 — hatua iliyozua hasira Nairobi. Sasa serikali ya Kenya imelazimika kuimarisha uhusiano na madola mengine yenye uchumi mkubwa duniani baada ya kubaini kuwa Marekani haiwezi aminika tena.
Waziri wa Nishati na Petroli Opiyo Wandayi amesema ujumbe wa Kenya utawasilisha fursa za uwekezaji na kuchunguza maeneo ya ushirikiano wa baadaye, hasa katika sekta ya nishati ambako China imekuwa na mchango mkubwa.

Ziara ya Ruto pia inatarajiwa kuweka mkazo katika miundombinu, mojawapo ya maeneo ya msingi ya ushirikiano wa pande mbili.
Kenya inaipa kipaumbele kukamilisha njia kuu za usafirishaji wa kikanda ili kurahisisha usafirishaji wa bidhaa, kupunguza gharama za biashara, na kuimarisha ujumuishaji wa kikanda.
Mradi mkubwa katika mpango huu ni uboreshaji wa barabara ya Rironi-Mau Summit, sehemu ya Korridori ya Kaskazini inayounganisha mji wa pwani wa Mombasa na nchi zisizo na bahara kama vile Uganda, Rwanda, Burundi na DRC.
Aidha Ruto anafuatilia upanuzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kutoka Naivasha hadi Malaba, karibu na mpaka wa Kenya na Uganda. Kwa kuwa China ilifadhili awamu za awali za SGR kutoka Mombasa hadi Nairobi na Naivasha, Kenya inatumaini kuwa China itaunga mkono kukamilika kwa njia hii muhimu ya usafirishaji.