Wanasheria: A/Kusini haina namna nyingine ila kuunga mkono Muqawama
Hatua ya Afrika Kusini ya kuongoza kampeni muhimu ya kisheria katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) dhidi ya mauaji ya umati yanayofanywa na Israel huko Ghaza ni ushahidi wa msimamo wa kishujaa wa nchi hiyo ya Afrika na wanasheria wanasema, Pretoria haina namna nyingine isipokuwa kuendelea kuwaunga mkono wananchi madhlumu wa Palestina.
Tarehe 29 Disemba 2023 imerekodiwa katika kumbukumbu za historia ya baada ya mwaka 1994 ya Afrika Kusini kama siku ambayo nchi hiyo ilifungua kesi dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel katika mahakama ya ICJ, ikiwasilisha hoja za kisheria za kina na zenye mashiko kwamba ukatili wa Israel katika Ukanda wa Ghaza unakanyaga Mkataba wa Kimataifa wa Kuzuia Mauaji ya Kimbari.
Hayo yamesisitizwa na timu ya wanasheria wa Afrika Kusini, iliyojumuisha wataalamu wa sheria za kimataifa. Timu hiyo imeiomba Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ yenye makao yake mjini The Hague Uholanzi kuchukua maamuzi ya kiuadilifu ya kuwatendea haki Wapalestina ambao wamedhulumiwa vibaya katika kipindi cha zaidi ya miaka 75 na kukomesha uvamizi wa Israel kwenye eneo hilo.
Tarehe 26 Januari 2024, ICJ iliiamuru Israel kuchukua hatua zote za kuzuia kufanyika vitendo vyote vilivyopigwa marufuku kwenye Ibara ya II ya Mkataba wa Mauaji ya Kimbari, na kuchukua hatua za haraka na madhubuti kuwezesha utoaji wa huduma za kimsingi zinazohitajika haraka kwa ajili ya wananchi wa Ghaza.
Kwa upande wake, Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini Naledi Pandor amesema kuwa, ni wazi kwamba kushindwa kusitishwa mashambulizi ya kimbari ya Israel kwenye Ukanda wa Ghaza kumefichua mapungufu ya mifumo ya kisheria ya kimataifa na kumeibua upya udharura wa kufanyiwa mageuzi ya kimsingi taasisi za kimataifa hasa Umoja wa Mataifa.