UN: Hukumu ya kesi ya "uhaini" nchini Tunisia ni pigo kwa haki na uadilifu
(last modified Fri, 25 Apr 2025 12:39:29 GMT )
Apr 25, 2025 12:39 UTC
  • Volker Türk
    Volker Türk

Umoja wa Mataifa umetaja hukumu zilizotolewa dhidi ya makumi ya watu wakiwemo viongozi wa upinzani katika kesi ya "njama dhidi ya usalama wa taifa" nchini Tunisia kuwa ni "kurudisha nyuma haki na utawala wa sheria," ukieleza kuwa kulikuwa na "matashi ya kisiasa" nyuma ya maamuzi hayo.

Kamishna Mkuu wa Haki za Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Türk amesema katika taarifa iliyotolewa na Tume ya Umoja wa Mataifa kwenye tovuti yake kwamba: "Hukumu kali na za muda mrefu za vifungo gerezani zilizotolewa hivi majuzi dhidi ya watu 37 nchini Tunisia katika kile kinachoitwa kesi ya kula njama dhidi ya usalama wa taifa, ni kurudisha nyuma haki na utawala wa sheria." 

Volker Türk amesema, "Kesi hiyo iligubikwa na ukiukwaji wa haki za kesi ya uadilifu na mchakato unaostahili, na hivyo kuzua wasiwasi mkubwa kuhusu kuwepo matashi ya kisiasa (katika maamuzi yake)."

Ameendelea kusema kuwa, "kesi hiyo ilikosa uwazi, kwani ushahidi haukuwasilishwa hadharani au kujaribiwa kwa kuhojiwa, na waandishi wa habari, wawakilishi wa mashirika ya kiraia na wanadiplomasia walizuiwa kuhudhuria vikao vya hadhara vya kesi hiyo."

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amesema, kabla ya kutolewa hukumu hizo, washtakiwa hawakupewa nafasi ya kuzungumza, na mawakili wao hawakupewa muda wa kutosha kuwasilisha hoja zao.

Turk ametoa wito wa "kuhakikisha kwamba washtakiwa wote wanapata haki zao kamili za mchakato unaostahili na kusikilizwa kesi hiyo katika mchakato wa kukata rufaa," na amesema, "mashtaka yanapaswa kufutwa ikiwa hakuna ushahidi wa kutosha wa madai yaliyowasilishwa."

Jumamosi iliyopita, Mahakama ya Tunisia iliwahukumu viongozi kadhaa wa upinzani, mawakili na wafanyabiashara vifungo vya kati ya miaka 13 hadi 66 jela kwa tuhuma za kula njama ya kuhatarisha usalama wa taifa.

Kesi hiyo ambayo imelaaniwa na mashirika ya kutetea haki za binadamu, haijawahi kushuhudiwa mfano wake kwa kuhusisha washtakiwa wapatao 40, miongoni mwao wakiwemo wakosoaji wakubwa wa Rais Kais Saied na utawala wake wa kimabavu.