UN yataka kukomeshwa mapigano mara moja Sudan Kusini
Timu ya Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini UNMISS imetoa mwito wa kukomeshwa mara moja mapigano baada ya kushadidi vita kati ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Sudan Kusini (SSPDF) na wanajeshi wa upinzani wanaomuunga mkono Makamu wa Kwanza wa Rais, Riek Machar.
Pande hizo mbili zimekuwa zikipigana tangu mwishoni mwa mwezi Februari huko Upper Nile kabla ya mapigano hayo kuenea hadi kwenye Jimbo la Equatoria ya Kati ambako idadi kubwa ya wanajeshi wa upinzani wa Jeshi la Ukombozi la Watu wa Sudan walikuwa wamewekwa.
Taarifa ya UNMISS iliyotolewa huko Juba, mji mkuu wa Sudan Kusini imesema: "Tunatoa mwito kwa wahusika wote wa kijeshi kujiepusha na migogoro, kutanguliza mbele ulinzi wa raia, kusuluhisha tofauti kwa njia ya mazungumzo na kuhakikisha amani na usalama unapatikana bila ya kuwekewa vizuizi vyovyote.
Timu hiyo ya Umoja wa Mataifa imesema kwamba ina wasiwasi mkubwa kutokana na kuongezeka mapigano kati ya pande hizo mbili hasimu katika kaunti za Morobo na Yei za Equatoria ya Kati, ambayo yamesababisha raia wengi kuhama makazi yao na wengine wengi kuuawa na kujeruhiwa.
Zaidi ya watu 7,000 wamekimbia makazi yao huko Morobo pekee tangu mapigano yalipozuka wiki iliyopita kati ya vikosi hivyo viwili.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, UNMISS inashirikiana kwa kina na serikali, vikosi vya usalama, viongozi wa kidini na wa kimila, mashirika ya kiraia, vijana na wanajamii ili kuzuia hali kuwa mbaya zaidi.
Mapigano kati ya pande hizo mbili yaliongezeka kufuatia mauaji ya wanajeshi 27 wa SSPDF ya tarehe 7 Machi huko Nasir, Jimbo la Upper Nile kulikofuatiwa na kukamatwa Machar na washirika wake kadhaa.