Nchi zenye wanajeshi wa AU zataka kuimarishwa usalama Somalia
(last modified Sat, 26 Apr 2025 11:09:26 GMT )
Apr 26, 2025 11:09 UTC
  • Nchi zenye wanajeshi wa AU zataka kuimarishwa usalama Somalia

Mawaziri wa ulinzi na mambo ya nje wa nchi zenye wanajeshi katika kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Afrika (AU) nchini Somalia wametoa mwito wa kuchukuliwa hatua za haraka za kuongeza idadi ya wanajeshi na kuimarisha usalama nchini Somalia kutokana na kuzidi kudorora hali ya usalama huku genge la kigaidi la al-Shabaab likizidi kuimarika.

Mawaziri hao kutoka Djibouti, Ethiopia, Kenya na Uganda, pamoja na wale wa Somalia wametoa mwito huo kwenye kikao chao cha mjini Kampala Uganda. Mawaziri wawili wa Misri nao wameshiriki kwenye kikao hicho.

Jacob Oboth, Waziri wa Ulinzi wa Uganda amesisitizia haja ya kukabiliana na tishio linaloongezeka la mashambulio ya al-Shabaab sambamba na kuimarishwa juhudi za kuleta utulivu wa kudumu nchini Somalia.

Vilevile ametoa mwito wa kuongezwa idadi ya wanajeshi wa kulinda amani, akionya kwamba kuna hatari ya kupoteza mafanikio ya kazi iliyofanyika kwa bidii kubwa huko Somalia kama askari zaidi hawatapelekwa kukabiliana na genge la al-Shabab.

Kwa upande wake, Ahmed Moallim Fiqi, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Somalia ametoa mwito wa kuimarishwa haraka vikosi vya kukabiliana na mashambulizi ya al-Shabaab akisema kuwa, amani nchini Somalia ina maana ya utulivu wa eneo zima la Pembe Afrika.

Mwezi Mei 2019, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipasisha azimio la kuidhinisha kupunguzwa idadi ya wanajeshi wa kulinda amani, huku vikosi vya Somalia vikichukua jukumu la kulinda usalama wa nchi yao. Uganda ilipunguza askari wake na Burundi iliondoa kabisa wanajeshi wake kutoka kwenye nchi hiyo yenye matatizo mengi hasa ya kiusalama.

Sambamba na kuzidi kuwa mbaya hali ya usalama nchini Somalia, Uganda ilitangaza mapema mwaka huu kwamba ina mpango wa kupeleka wanajeshi zaidi nchini humo. Misri pia imeonesha nia ya kupeleka wanajeshi wake nchini Somalia.

Naye Mahmoud Ali Youssouf, mwenyekiti wa Kamisheni ya AU, ametilia mkazo haja ya kuweko uungaji mkono endelevu wa kisiasa na kifedha kwa ajili ya kazi za AU nchini Somalia.