Mashambulizi ya ndege za Marekani nchini Libya yalaaniwa na jeshi la serikali
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i12580-mashambulizi_ya_ndege_za_marekani_nchini_libya_yalaaniwa_na_jeshi_la_serikali
Jeshi la Libya limelaani mashambulizi ya anga ya ndege za kijeshi za Marekani katika mji wa Sirte nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 04, 2016 03:17 UTC
  • Mashambulizi ya ndege za Marekani nchini Libya yalaaniwa na jeshi la serikali

Jeshi la Libya limelaani mashambulizi ya anga ya ndege za kijeshi za Marekani katika mji wa Sirte nchini humo.

Ahmed al-Mismari, msemaji wa askari wa serikali isiyo rasmi yenye makao yake mjini Bengazi, mashariki mwa nchi hiyo na wanaoongozwa na kamanda Khalifa Haftar amewambia wandishi wa habari kuwa, mashambulizi hao ya anga ya ndege za Marekani yanakiuka sheria na yamefanyika bila ya idhini ya bunge la nchi hiyo. Al-Mismari amesema kuwa, mji wa Sirte umegeuka na kuwa karatasi ya kisiasa ambayo ina nafasi muhimu na kubwa katika uchaguzi wa rais nchini Marekani na Libya pia. Ameongeza kuwa, jambo hilo limekuwa na taathira mbaya dhidi ya serikali ya umoja wa kitaifa nchini Libya chini ya Fayez al-Sarraj, Waziri Mkuu wa nchi hiyo.

Msemaji wa askari wa serikali isiyo rasmi yenye makao yake mjini Bengazi amesema kuwa, mashambulizi hayo ya anga ya Marekani yametekelezwa kwa malengo ya kisiasa. Itakumbukwa kuwa Jumatatu iliyopita na kwa mujibu wa kile kilichoelezwa kuwa ni takwa la serikali ya umoja wa kitaifa na Umoja wa Mataifa, Marekani ilianzisha mashambulizi ya anga dhidi ya ngome za wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh mjini Sirte, kaskazini mwa Libya. Siku moja baadaye Rais Barack Obama wa Marekani alitetea mashambulizi hayo na kudai kuwa, kuwashinda magaidi hao huko Libya ni kwa maslahi ya taifa la Marekani.