Sudan: Waasi wa RSF wameua raia zaidi ya 300 Kordofan
Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan imevituhumu Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) kwa kufanya "mauaji ya halaiki" dhidi ya raia huko Al-Nahud katika jimbo la Kordofan Magharibi, kusini mwa nchi na kusababisha vifo vya watu 300.
RSF ilikuwa haijatoa taarifa yoyote kuhusu tuhuma hizo lakini kundi hilo lilitangaza kuwa limechukua udhibiti wa El-Khuwei huko Kordofan Magharibi, siku moja baada ya kuiteka Al-Nahud kusini mwa Sudan.
"Wanamgambo wa RSF wanaendelea kufanya uhalifu dhidi ya binadamu, mauaji ya halaiki, na mauaji ya kimbari katika maeneo mbalimbali ya nchi," Wizara ya Mambo ya Nje imesema katika taarifa.
Taarifa hiyo imeeleza, "Katika muda wa siku mbili zilizopita, wanamgambo hao wamefanya jinai mpya za kutisha dhidi ya raia katika mji wa Al-Nahud, ambapo wamefanya mauaji ya halaiki kwa misingi ya kikabila. Idadi ya waliouawa hadi sasa imepindukia watu 300."
Wizara hiyo kwa mara nyingine tena imelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na wahusika wa kimataifa kuacha kuacha kufumbia macho jinai zinazofanywa na wanamgambo wa RSF.
RSF ilitangaza Ijumaa iliyopita kwamba, imechukua udhibiti kamili wa Al-Nahud na kuteka makao makuu ya Brigedi ya 18 ya Jeshi la wanaotembea kwa miguu katika jiji hilo, kufuatia mapigano makali baina ya pande mbili.
Kabla ya hapo, msemaji wa jeshi la Sudan alitangaza kuwa, wanamgambo wa RSF wamefanya shambulio la ndege isiyo na rubani (droni) katika kambi ya jeshi la nchi hiyo na katika vituo vingine karibu na uwanja wa ndege wa Port Sudan. Hilo ni shambulio la kwanza kuwahi kufanywa na wanamgambo wa RSF katika mji huo wa bandari wa mashariki.