Baraza la Usalama laongeza muda wa kuhudumu UNMISS Sudan Kusini
(last modified Fri, 09 May 2025 10:35:48 GMT )
May 09, 2025 10:35 UTC
  • Baraza la Usalama laongeza muda wa kuhudumu UNMISS Sudan Kusini

Baada ya majuma kadhaa ya mazungumzo makali, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeongeza muda wa kikosi cha kulinda amani nchini Sudan Kusini, UNMISS, kwa mwaka mmoja mwingine, huku likitaka kusitishwa mara moja kwa mapigano kati ya pande hasimu.

Ujumbe huo, ambao unaweza kujumuisha hadi wanajeshi 17,000 na maafisa wa polisi 2,100, unaweza kurekebisha idadi na kazi zake kulingana na hali ya usalama nchini Sudan Kusini.

Idadi kubwa ya wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, likiongozwa na Marekani, hawajaridhishwa na jinsi serikali ya mpito inavyoshughulikia UNMISS nchini Sudani Kusini na wanahofia kwamba kikosi cha Umoja wa Mataifa hakitaweza kutekeleza jukumu lake la kuleta utulivu. Hatari ya Sudani Kusini kurejea kwenye mzozo wa kikabila bado iko juu kutokana na kuanza kwa mapigano, amesema Kaimu Balozi wa Marekani Dorothy Shea. Baadhi ya wajumbe wa Baraza pia wameitaka serikali ya mpito kuacha kuzuia kazi ya UNMISS kwa kuweka vikwazo vya usafiri.

Huku hayo yakiripotiwa, bado kungali kuna mvutano mkubwa wa kisiasa na kiusalama kufuatia hatua ya Riek Machar kuwekwa kizuizini tarehe 26 Machi, katika hali ambayo inaripotiwa kutishia mpango wa 2018 uliomaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka mitano.

Chini ya mkataba huo uliotiwa saini mwaka wa 2018, serikali ya umoja wa kitaifa na mpito iko mjini Juba. Rais Salva Kiir na mpinzani wake wa muda mrefu, Makamu wa Rais Riek Machar, waligawana madaraka. Hata hivyo tangu mwanzoni mwa mwaka, makabiliano ya moja kwa moja kati ya vikosi vyao hasimu vya kijeshi yameripotiwa katika mikoa kadhaa.