Makumi wauawa katika mashambulizi ya wabeba silaha Benue, Nigeria
(last modified Mon, 12 May 2025 11:10:52 GMT )
May 12, 2025 11:10 UTC
  • Makumi wauawa katika mashambulizi ya wabeba silaha Benue, Nigeria

Takriban watu 23 waliuawa huku wengine wengi kujeruhiwa katika mashambulizi ya watu waliojizatiti kwa silaha katika Jimbo la Benue nchini Nigeria.

Ofisa wa Serikali ya Mtaa wa Kwande, Ray Anuve, katika mahojiano yake na gazeti moja la Nigeria jana Jumapili aliwatuhumu wafugaji wa jamii ya Fulani kuwa ndio waliofanya mashambulizi hayo katika vijiji vya jimbo hilo la kaskazini ya kati ya nchi.

Anuve amethibitisha kuwa watu 23 waliuawa, wakiwemo watoto wadogo. Amesema kuwa nyumba kadhaa pia zilichomwa moto wakati wa mashambulizi hayo na kwamba washambuliaji walipora chakula cha wanakijiji.

Wafugaji wa kabila la Fulani wanaohama katika mikoa mbalimbali nchini humo kutafutia mifugo yao lishe, wamedai kuwa wakulima wa vijiji hivyo walijaribu kuiba mifugo yao ndiposa wakawashambulia.

Kwa muda mrefu sasa, kumekuwa na mapigano ya mara kwa mara kati ya wafugaji wa Fulani na jamii zinazojihusisha na kilimo jimboni Benue.

Katika shambulio kama hilo mwezi uliopita wa Aprili, karibu watu 100 waliuawa katika jimbo hilo la Benue. Magenge yenye silaha yametumia vibaya migogoro hii, na kuanzisha mashambulizi na kutishia wakazi wa eneo hilo.