Profesa Janabi ashinda kiti cha Mkurugenzi wa WHO Afrika
Profesa Mohammed Janabi kutoka Tanzania ameshinda uchaguzi wa kuwania kuwa Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Kanda ya Afrika.
Katika uchaguzi uliofanyika Geneva nchini Uswisi, Janabi alikuwa akichuana na wenzake wanne, Dk. N’da Konan Yao wa Ivory Coast, Dk Drame Lamine wa Guinea, Dk Boureima Sambo wa Niger na Prof. Mijiyawa Moustafa kutoka Togo.
Sasa ni rasmi Tanzania imetoa mkurugenzi mwingine katika nafasi hiyo, baada ya awali, Dk. Faustine Ndugulile aliyeshinda, kufariki dunia kabla hajaanza kutumikia rasmi nafasi hiyo.
Kuchaguliwa kwake kunakuja baada ya kifo cha aliyekuwa amechaguliwa awali, Dkt. Faustine Ndugulile pia kutoka Tanzania, ambaye alifariki ghafla Novemba 2024, muda mfupi kabla ya kuanza rasmi majukumu yake.
Profesa Janabi, ambaye ni mtaalamu wa magonjwa ya moyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, mshauri wa Rais Samia Suluhu kwenye eneo la afya na daktari wa rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete, amekuwa na mchango mkubwa katika sekta ya afya nchini Tanzania
Baada ya ushindi huu, jina la Profesa Janabi litathibitishwa na kikao cha 157 cha Bodi ya Utendaji ya WHO, kitakachofanyika kuanzia tarehe 28 hadi 29 Mei 2025 huko Geneva. Kwa mujibu wa utaratibu Janabi atahudumu kwa kipindi cha miaka mitano lakini anaweza kuteuliwa tena kuhudumu kipindi kingine cha miaka mitano.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika ana jukumu la kuongoza na kusimamia shughuli zote za WHO katika nchi 47 wanachama wa kanda hiyo.
Majukumu haya ni pamoja na kutoa mwelekeo wa kimkakati kwa programu za afya, kuratibu juhudi za kukabiliana na dharura za kiafya kama vile milipuko ya magonjwa, na kuhakikisha usawa katika ugawaji wa rasilimali na huduma za afya katika kanda.