Kenya yasema kurudishwa nyumbani Karua hakutaathiri uhusiano na Tanzania
(last modified Mon, 19 May 2025 11:40:48 GMT )
May 19, 2025 11:40 UTC
  • Kenya yasema kurudishwa nyumbani Karua hakutaathiri uhusiano na Tanzania

Msemaji wa serikali ya Kenya amesema kuwa kuondoshwa kwa Martha Karua nchini Tanzania hakutavuruga uhusiano wa kidiplomasia kati ya Kenya na Tanzania.

Karua, ambaye aliwahi kuwa waziri na mgombea urais, alikuwa amekwenda kuhudhuria kesi ya Tundu Lissu lakini akazuiwa kuingia na kurudishwa Nairobi. Serikali ya Kenya imesema inatilia mkazo umuhimu wa kuheshimu sheria za nchi nyingine, huku ikisisitiza kuwa tukio hilo halimaanishi kuwpo mzozo wa kidiplomasia.

Msemaji wa serikali ya Kenya Issac Mwaura amesema kuwa nchi hizi mbili ni wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na kila moja ina njia yake ya kushughulikia mambo. Amesema kila serikali ina haki ya kumzuia mtu yeyote kuingia katika ardhi yake na kuongeza kuwa uhuru wa mipaka haumaanishi tahadhari zisichukuliwe. Wanaharakati wengine kadhaa wa Kenya pia wamezuiwa kuingia Tanzania akiwemo jaji mkuu mstaafu Willy Mutunga.

Pamoja na hayo jaji mkuu mstaafu mwingine wa Kenya David Maraga ni miongoni mwa watu Mashuhuri waliofika mahakamani Kisutu, Dar es Salaam Tanzania, kuhudhuria kesi Lissu. Kesi hiyo imewavutia wanaharakati wa haki za binadamu na vilevile mabalozi wa nchi za kigeni.

Kesi ya uhaini dhidi ya Lisu ilipotajwa, upande wa Jamhuri umeieleza Mahakama kuwa upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika na wameiomba Mahakama kuahirisha kesi husika kwa siku 14 zaidi, jambo ambalo limepingwa vikali na mawakili wa utetezi.

Kesi hii imeahirishwa hadi Juni 2 mwaka huu ambapo itasikilizwa kwa njia ya mahakama ya wazi na shauri la uchochezi dhidi ya Lisuu kadhalika bado linaendelea.

Lissu alikamatwa Aprili 9 baada ya kuitisha mageuzi ya uchaguzi na kuhimiza kususiwa uchaguzi ujao wa Oktoba. Anakabiliwa na mashtaka ya uhaini na kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni, ikiwa ni pamoja na madai kwamba alichochea uasi na kuwashutumu polisi kwa utovu wa nidhamu katika uchaguzi.