Miili 105 ya wahamiaji 'haramu' iliopolewa katika pwani ya Senegal 2024
Jumla ya miili 105 iliopolewa kutoka baharini pwani ya Senegal mwaka 2024 baada ya kupinduka kwa mitumbwi yao iliyohusishwa na uhamiaji 'usio wa kawaida'.
Modou Diagne, Katibu Mkuu wa Kamati ya Mawaziri ya Senegal ya Kupambana na Uhamiaji Wasio wa Kawaida, amesema hayo na kuongeza kuwa, "Idadi hii haijumuishi wale ambao bado miili yao ipo chini ya bahari."
Diagne amesema hayo wakati wa hafla ya uzinduzi wa kamati za kikanda na idara za kupambana na uhamiaji haramu huko Diourbel, katikati mwa Senegal.
Pwani za Senegal hutumiwa mara kwa mara na wahamiaji wa Kiafrika wanaoelekea katika Visiwa vya Canary vya Uhispania, ambavyo vinatumika kama moja ya maeneo makuu ya watu wanaojaribu kufika Ulaya.
Diagne ametoa wito wa kuimarishwa kwa kampeni za uhamasishaji kwa vijana. Mamia ya wahajiri wanapoteza maisha kila mwaka kutokana na ajali za boti na mitumbwi, wakiwa katika safari hatarishi za baharini kuelekea Uhispania na nchi nyingine za Ulaya kupitia Bahari ya Atlantic .
Wahamiaji wenye ndoto za kuingia Ulaya ambao wengi wao ni kutoka Afrika Magharibi wameongezeka tangu mwaka 2023, ikilinganishwa na mwaka 2020 hadi 2022 wakati wa janga la Corona.
Hata hivyo sehemu kubwa ya wahamiaji hao haramu huwa hawafiki wanakokwenda, bali huishia kwenye mikono ya magenge ya magendo ya binadamu na kupigwa mnada masokoni kama watumwa na sehemu nyingine kubwa huzama baharini.
Hivi karibuni, Rais wa Senegal, Bassirou Diomaye Faye alisema kuwa serikali yake itafanya kila liwezekanalo kukabiliana na safari hizo hatarishi za wahamiaji baada ya mkasa wa karibuni kuua mamia ya watu.