Namibia yataka fidia ya 'maana' ya mauaji ya halaiki ya Ujerumani
(last modified Thu, 29 May 2025 06:01:24 GMT )
May 29, 2025 06:01 UTC
  • Namibia yataka fidia ya 'maana' ya mauaji ya halaiki ya Ujerumani

Namibia imefanya kumbukizi ya kuwaenzi wahanga wa mauaji ya kibari wakati wa utawala wa kikoloni wa Ujerumani, huku viongozi, wanasiasa na wakuu wa jamii zilizoathirika na ukatili huo wa askari wa Kijerumani wakitoa wito mpya wa kulipwa fidia na Berlin.

Rais wa Namibia, Netumbo Nandi-Ndaitwah aliuambia umati uliohudhuria kumbukumbu hiyo katika Bustani ya Bunge jijini Wndhoek jana Jumatano kwamba, "Tunapaswa kupata kiasi cha faraja kutokana na ukweli kwamba, serikali ya Ujerumani imekiri kuwa wanajeshi wake walifanya mauaji ya halaiki."

Mwaka 2021, Ujerumani kwa mara ya kwanza ilikiri rasmi kuwa mauaji ya enzi za ukoloni yalikuwa ya halaiki, na kukubali kufadhili miradi ya maendeleo yenye thamani ya euro bilioni 1.1 (dola bilioni 1.2) katika nchi hiyo ya Kusini mwa Afrika, lakini ikapuuzilia mbali suala la kutoa fidia.

"Huenda tusikubaliane juu ya kiasi cha mwisho, lakini hiyo ni sehemu ya mazungumzo tata ambayo tumekuwa tukifanya na serikali ya Ujerumani tangu 2013," amesema Rais wa Namibia.

Jeshi la Ujerumani liliuwa makumi ya maelfu ya watu wa jamii za Herero na Nama wakati wa ghasia za kupinga ukoloni. Wanajeshi wa Ujerumani waliwaua Waherero 65,000 na Wanama 10,000 mnamo 1904-1908, katika kile wanahistoria na Umoja wa Mataifa wameita mauaji ya kwanza ya kimbari katika karne ya 20.

Charles Kakomee Tjela, mjukuu wa wahanga wa mauaji hayo ya halaiki aliohudhuria hafla hiyo katika Bustani ya Bunge, aliiambia Reuters kwamba, mauaji hayo ya halaiki yanapaswa kuakisiwa zaidi katika mitaala ya shule.
Kwa upande wake, Hoze Riruako, chifu wa jamii ya OvaHerero, alisema ukatili wa enzi za ukoloni ulikuwa utangulizi wa mauaji ya 'Holocaust' lakini "watu hawajui kilichotokea hapa kwa undani." Naye McHenry Venaani, kiongozi wa upinzani nchini humo amesisitiza kuwa, kiasi cha awali cha fidia kilichopendekezwa na Ujerumani ni kidogo mno, hakitoshi.