WFP: Mamilioni ya raia wa Sudan wanakabiliwa na janga la njaa
Mamilioni ya wakimbizi wa Sudan wanakabiliwa na janga la njaa huku uhaba mkubwa wa fedha ukilazimisha Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) kupunguza msaada muhimu unaoweza kuokoa maisha ya mamilioni ya raia wa nchi hiyo.
Onyo la WFP linakuja wakati huu ambapo zaidi ya raia milioni 4 wa Sudan wakiwa wamekimbilia katika mataifa jirani tangu kuzuka kwa mapigano mwezi Aprili mwaka wa 2023.
Aidha WFP inasema kuwa, idadi kubwa ya wakimbizi wanaotoka Sudan na kuingia katika nchi jirani wanakabiliwa na utapiamlo pamoja na msongo wa mawazo na kwamba huenda misaada wanayopata ikaisha katika kipindi cha miezi michache ijayo.
Kwa sasa WFP inatoa wito wa msaada wa zaidi ya Dolla Milioni 200 kuwasaidia wakimbizi kwenye nchi za Ukanda.
Mataifa yanayowapa hifadhi wakimbizi hao kama vile Uganda, Chad, Libya, Ethiopia na Jamhuri ya Afrika ya Kati, tayari yameanza kuripoti kutoa chakula kwa mgao, Misri ambayo inatoa hifadhi kwa karibia wakimbizi Milioni 1.5 wa Sudan ikiripotiwa kuathirika zaidi.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, idadi ya wakimbizi inazidi kuongezeka kila siku kutokana na ukosefu wa amani nchini Sudan.
Wakimbizi kutoka Sudan wanaingia katika nchi jirani ya Sudan Kusini katika hali ambayo Sudan Kusini yenyewe ina mzigo wa wakimbizi wa ndani.
Wakimbizi hao wanaowasili huko Sudan Kusini na wakimbizi wa ndani wa nchi hiyo wanakabiliwa na hali mbaya katika kambi za wakimbizi kutokana na uhaba wa huduma mbalimbali.
Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, mashirika ya misaada ikiwemo jumuiya ya misaada ya kibinadamu nchini Sudan Kusini, yanatafuta ufadhili wa haraka wa kuwasafirisha watu wanaokimbia mapigano nchini Sudan.