Waislamu nchini Nigeria waandamana kutaka Sheikh Ibrahim Zakzaky aachiliwe huru
Waislamu nchini Nigeria wameendelea kufanya maandamano ya amani wakitaka kuachiliwa huru Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya nchi hiyo aliyewekwa kizuizini na vikosi vya usalama vya nchi hiyo.
Kama ilivyokuwa katika siku za nyuma, leo pia miji kadhaa ya nchi hiyo ilishuhudia maandamano ya kutaka kuchiliwa huru Sheikh Ibrahim Zakzaky.
Waandamanaji hao wakiwa wamebeba mabango na maberamu walipiga nara za kutaka kuachiliwa huru mwanazuoni huyo wa Kiislamu ambaye amekuwa kizuizini kwa miezi minane sasa.
Waandamanaji hao wameitaka serikali ya Nigeria kumtendea haki Sheikh ibrahim Zakzaky na kumuachilia huru.
Waandamanaji hao wamesikika wakipiga nara kwa kusema: "Ima mauti au Sheikh Zakzaky" wakitangaza wazi kwamba, wako tayari kufa kwa ajili ya kumtetea kiongozi huyo wa Harakati ya Kiislamu nchini Nigeria yenye makao yake mjini Zaria.
Hayo yanaripotiwa katika hali ambayo, baadhi ya ripoti zinasema kuwa, hali ya kiafya ya Sheikh Ibrahim Zakzaky ni mbaya sana.
Watu waliokutana na Sheikh Zakzaky gerezani hivi karibuni walisema jicho lake la kushoto limepofuka na kwamba maafisa usalama wamekuwa wakizuia mwanazuoni huyo wa Kiislamu kupatiwa matibabu.
Wananchi wa Nigeria wamekuwa wakiandamana katika miji mbalimbali ya nchi hiyo wakitaka kuachiwa huru haraka kiongozi huyo wa Kiislamu. Itakumbukwa kuwa tarehe 12 Disemba mwaka jana askari wa jeshi la Nigeria walishambulia marasimu ya kidini ya Waislamu wa Kishia katika mji wa Zaria kwa kuwatuhumu kuwa walizuia msafara wa mkuu wa jeshi na pia kujaribu kumuua, madai ambayo yalikanushwa na Waislamu hao.