Ethiopia yazindua kampeni ya kupanda miti milioni 700 kwa siku moja
Ethiopia imezindua kampeni ya ustawishaji wa mazingira ambayo haijawahi kushuhudiwa wakati mamilioni ya wananchi waliposhiriki jana Alkhamisi katika juhudi za kitaifa za kupanda miti milioni 700 kwa siku moja.
Mpango huo kabambe ni sehemu ya mkakati wa Waziri Mkuu Abiy Ahmed wa Urithi wa Kijani, ambao unalenga kuhakikisha hadi ifikapo mwaka 2026 miti bilioni 50 iwe imekwishapandwa katika taifa hilo lenye tatizo la ukame.
Kulipopambazuka mapema jana, Waethiopia kutoka matabaka mbalimbali walionekana wakichimba na kupanda miche ya miti katika maeneo ya mijini na kwenye mandhari za mashambani.
Msemaji wa serikali Tesfahun Gobezay ameripoti kuwa, wananchi milioni 14.9 walikuwa tayari wameshapanda miche milioni 355 kabla ya saa 12 asubuhi kwa saa za huko, ingawa takwimu hizo hazikuweza kuthibitishwa wakati huo na duru huru.
Waziri Mkuu Abiy, ambaye ameongoza mradi huo wa upandaji miti tangu mwaka 2019, alitumia jukwaa la kijamii la X kuhamasisha ushiriki akisema: "tumezindua kampeni ya kila mwaka ya upandaji miti wa Urithi wa Kijani mapema leo asubuhi. Lengo letu mwaka huu ni miche milioni 700. Shime tufanikisheni kwa pamoja".
Mshindi huyo wa Tuzo ya Amani ya Nobel alijiunga na shughuli za upandaji miti huko Jimma, jiji kubwa zaidi kusini magharibi mwa mkoa wa Oromia, wakati mawaziri wake walijitokeza katika majimbo mengine kuunga mkono kampeni hiyo.../