EALA kusuluhisha uhasama kati ya Rwanda na Burundi
(last modified Tue, 09 Aug 2016 13:11:35 GMT )
Aug 09, 2016 13:11 UTC
  • EALA kusuluhisha uhasama kati ya Rwanda na Burundi

Bunge la Afrika Mashariki EALA limesema karibuni hivi litaanza kuchunguza kwa shabaha ya kuupatia ufumbuzi mzozo na uhasama kati ya nchi jirani za Rwanda na Burundi.

Daniel Kidega, Spika wa bunge hilo la kikanda amesema EALA itaanzisha uchunguzi huru ili kubaini kiini cha mivutano na uhasama kati ya nchi mbili hizo na kisha kuwasilisha mapendekezo yao kwa viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC ili watoe muelekeo zaidi.

Ramani inayoonyesha mpaka wa Burundi na Rwanda

Amesema kuwa ni jambo la kusikitisha kuona nchi mbili hizo zinawekeana vikwazo vya kibiashara pamoja na vizingiti vya kuingia na kutoka katika nchi hizo miongoni mwa raia wao, licha ya kusainiwa protokali ya kuimarisha ushikiriano wa kibiashara kati ya nchi wanachama wa EAC.

Bendera za nchi wanachama wa EAC

Kauli ya Spika wa Bunge la Afrika Mashariki imejiri baada ya serikali ya Bujumbura kuzuia bidhaa za Rwanda kuingizwa nchini Burundi kutokana na kushadidi uhasama kati ya nchi mbili hizo. Aidha polisi ya Burundi imetangaza kuwa imechukua hatua kali za kiusalama, kwa ajili ya kuwatathmini wanaoingia na kutoka katika maeneo ya mipaka yake na jirani yake Rwanda. Hii ni katika hali ambayo viongozi wa chama tawala nchini Burundi CNDD-FDD wanazituhumu baadhi ya nchi za Ulaya kwamba, zimekuwa zikiyapa misaada ya kifedha na silaha makundi ya waasi wa nchi hiyo ili kuyaandaa kufanya uasi dhidi ya serikali ya Bujumbura.

Hata hivyo tuhuma hizo zimekuwa zikikanushwa vikali na viongozi wa serikali ya Kigali, ambapo hivi karibuni ilitishia kuwatimua wakimbizi wote wa Burundi walioko nchini humo. 

Tags