Aug 10, 2016 03:38 UTC
  • Watu 5 wauawa katika mapigano Mali, askari 5 watoweka

Kwa akali watu watano wameuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa katika mapigano makali yaliyojiri kati kati ya Mali, huku duru za kiusalama zikiarifu kuwa askari watano wa serikali wametoweka baada ya kujiri mapigano hayo.

Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Mali, Diarran Kone, amethibitisha kutokea mapigano hayo mapya yaliyojiri baada ya kundi la kigaidi la Ansaruddin kushambulia mkusanyiko wa wanajeshi wa nchi hiyo.

Askari wa kusimamia amani wa Umoja wa Mataifa nchini Mali

Naye Souleymane Maiga, msemaji wa jeshi la nchi hiyo amesema mapigano hayo yalianza Jumapili alasiri katika kijiji cha Tenenkou eneo la Mopti na kwamba mbali na kutojulikana hatima ya askari watano wa nchi hiyo, wengine kadhaa walipata majeraha mabaya.

Kundi hilo la kigaidi limekiri kuhusika na hujuma hiyo dhidi ya maafisa usalama wa Mali na kuongeza kuwa, wametoweka na silaha na magari kadhaa ya jeshi hilo.

Rais Ibrahim Boubacar Keita

Kutokana na kushadidi wimbi la machafuko na kushambuliwa maafisa usalama wakiwemo askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Mali, Rais Ibrahim Boubacar Keita wa nchi hiyo Jumatano iliyopita alitangaza kurefusha hali ya hatari ambayo imedumu kwa miezi mitatu sasa.

Nchi ya Mali imekuwa ikikumbwa na mashambulizi ya makundi ya wabeba silaha katika maeneo ya kaskazini, tangu taifa hilo lilipokumbwa na mapigano ya mwaka 2012 na sasa maeneo ya katikati mwa nchi hiyo yamegeuka na kuwa uwanja wa machafuko. 

Tags